23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONDA ATAWAFIKIA MAPAPA WA UNGA?

Na AGATHA CHARLES – Dar es Salaam

ORODHA ya askari polisi 17, wasanii na watu mbalimbali 18 waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wiki hii katika sakata la dawa za kulevya, itasaidia kuwanasa watumiaji, wasambazaji na wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya nchini?

Hili ni swali ambalo sasa linaonekana kuumiza vichwa vya watu wengi, hasa ikizingatiwa kwamba suala hilo bado lipo chini ya uchunguzi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Miongoni mwa askari hao, 12 tayari wamesimamishwa kazi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu ili kupisha uchunguzi wa jambo hilo.

Ni uchunguzi huo ndio utakaobaini sababu za wao kutajwa katika sakata hilo la dawa za kulevya kama ambavyo alibainisha Makonda wiki hii.

Kusimamishwa kazi kwa askari hao na kuwekwa chini ya ulinzi katika Kituo Kikuu cha Polisi, wasanii na watu kadhaa kwa mahojiano, wapo ambao wanadhani kwa vyovyote kutaliwezesha Jeshi la Polisi kupata taarifa zaidi.

Wasanii waliotajwa na ambao walikuwa wameripoti polisi tangu juzi kwa mahojiano, ni pamoja na Wema Sepetu, Hamidu Chambuso ‘Dogo Hamidu’, Khalid Mohamed ‘TID’ na Babuu wa Kitaa.

Kabla ya hapo, mwanzoni mwa wiki hii wakati akitangaza orodha hiyo kwa mara ya kwanza, Makonda alisema alikuwa amewaweka ndani Ahmed Hashim Ngahemela (Petit Man), Said Masoud Lina (Alteza), Nassor Mohamed Nassor , Bakari Mohamed Khelef na Omar.

Katika orodha hiyo ya wasanii na watu mbalimbali, akiwamo Vanessa Mdee, mrembo anayependezesha video za muziki, Tunda na wengine wanne ambao watapaswa kufika kituoni kesho kutokana na wito wa Makonda nao huenda wakazalisha taarifa nyingine mpya.

Si hilo tu uchunguzi dhidi ya askari, watu na wasanii waliotajwa katika orodha hiyo, pia unaweza kuthibitisha au kutothibitisha tuhuma zinazowakabili.

Iwapo watapatikana baadhi ya wanaotumia, au wanaouza dawa hizo, ni dhahiri kuwa upo uwezekano wa kuwataja wanaowauzia au kufanya nao biashara hiyo na hatimaye katika mlolongo huo yatafikiwa majina ya vigogo wakubwa wa biashara hiyo.

Endapo hilo litafanikiwa, litafuta madai dhidi ya Makonda kuwa ameamua kuwaacha mapapa na kukamata vidagaa wa dawa hizo.

Juzi, Makonda kwa maneno yake alisema: “Kuwahoji hawa itatusaidia mambo mawili, kuna mwingine anasema ameacha, lakini anasema hakumbuki alipochukua, basi kama unatumia unajua yanapouzwa, kama hujui unapata wapi maana yake wewe unatengeneza dawa, ukitengeneza dawa ukaitumia mwenyewe haina shida ukiisambaza tunakutafuta.”

Ismail Juma, mkazi wa Magomeni, alisema endapo harakati hizo za Makonda zitafanikisha kujulikana na kuwataja kwa majina vigogo wa unga, wakiwamo wale ambao wamekuwa wakinyooshewa vidole na wananchi, atajijengea si tu heshima bali uaminifu mkubwa na kuandika historia mpya kwa taifa hili baada ya wengi kugwaya kufichua wanamtandao huo.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa mwaka 2006 kupitia Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete aliwahi kupatiwa orodha ya majina 58 wakiwamo polisi 20 na baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa, waliotajwa na wananchi kuwa wanajihusisha na mtandao wa dawa za kulevya.

Kikwete hadi anaondoka madarakani Novemba 5, mwaka juzi, hakuwahi kutaja kwa majina watu wanaojishughulisha na biashara hiyo licha ya mara kadhaa kudai kuwa alikuwa na orodha ndefu ya watu hao.

Ikulu yake iliwahi kusema kuwa orodha hiyo alikuwa ameikabidhi kwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Mwaka 2013, akiwa na wadhifa wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu), William Lukuvi, akiwa bungeni alisema iwapo akitaja majina ya wauza unga basi hata humo bungeni hawatapona.

Alipostaafu aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, aliwahi kukiri kutikiswa na baadhi ya vigogo wa dawa hizo.

Nzowa aliwahi kuliambia MTANZANIA Jumapili kuwa mmoja wa waliomtikisa ni bilionea Mtanzania anayedaiwa kuwa kinara wa mtandao wa dawa za kulevya, Ali Khatib Haji Hassan maarufu kama Shikuba (47) ambaye baadaye alikamatwa baada ya Marekani kutangaza kutaifisha mali zake.

Katika hilo, Nzowa alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa wauza unga hao waliwahi kutishia kumuua baada ya kugoma kupokea rushwa ya Sh bilioni 3 ili kuwaacha wapange mikakati na watuhumiwa wakuu wa dawa hizo aliokuwa amewakamata.

Nzowa alidai kuwa tukio hilo lilipangwa kufanyika akiwa nchini Kenya alikokwenda kuhudhuria mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi.

Mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kabla Rais Dk. John Magufuli hajamtoa kwenye nafasi yake, alipata kigugumizi kuweka hadharani orodha ya majina ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, licha ya kuliagiza Jeshi la Polisi limpatie kwa kusema kuwa jambo hilo halitasaidia kukomesha biashara hiyo.

Kutokana na hayo, mtihani mkubwa unaoelezwa kwa Makonda dhidi ya vita aliyoianzisha ni namna ya kuwafikia mapapa hao

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles