25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

ACHA TAMAA, JIFUNZE KURIDHIKA

KWA kawaida mwanzo wa uhusiano, huba na kila aina ya manjonjo kwenye mapenzi hutawala. Huwa na vitu vingi sana vya kuvutia, visivyochosha. Ni rahisi kuwasikia wenzi wakilaumiana kwa kutokuamshana asubuhi na mambo mengine madogomadogo.

Hiyo ni kwasababu mapenzi bado yanakuwa na matamu na mshawasha wa hali juu. Lakini ukweli ni kwamba, hayo ni mambo ya mwanzo. Ni ukweli ulio wazi kuwa, katika siku za mwanzo za wapenzi kukutana na kufahamiana, kila mmoja huwa makini kuhakikisha hamuudhi mwenzake.

Kila kitu hufanyika kwa umakini huku akizingatia kuwa kuna mtu mwingine katika maisha yake. Hataki kumkwaza mtu ambaye ndiye furaha yake. Kwa maneno mengine, kuchukia kwake, kutamfanya hata yeye akose furaha pia.

Hiyo ndiyo sababu kubwa hasa zinazowafanya wengi kuwa makini na uhusiano kuwa wenye nguvu. Ilivyo ni kwamba, baadaye uhusiano ukishachangamka na kufikia angalau mwaka mmoja au zaidi, kuna mambo yatabadilika.

Tayari hawa ni marafiki wakubwa, ambao kwa namna moja au nyingine wanafahamiana kwa karibu zaidi na pengine wameshaanza kuzoeana sasa. Marafiki, huo ndiyo ukweli wenyewe ulivyo.

Mfano niliotoa hapo juu, unafanana kabisa na hata kwa upande wa wanandoa. Siku za mwanzo wa ndoa huwa kuna vitu vinakuwa na mguso na mvuto wa aina yake lakini siku zinavyozidi kwenda, ndivyo baadhi ya mambo huanza kubadilika taratibu.

Ni mfumo. Hakuna cha ajabu. Hata hivyo, yapo mambo ambayo hupaswa kuzingatiwa ili penzi liendelee kudumu. Kweli kuna kupishana baadhi ya maeneo lakini sasa yasisababishe maisha yashindwe kuendelea mbele.

Zingatia maisha ni mtindo ambao huchaguliwa na mhusika mwenyewe. Kwa mfano, ukiamua kumnunia mkeo au mumeo kwasababu amefanya jambo fulani ni sawa na kulazimisha ‘stress’ ambazo si za lazima.

Kwanini usishughulikie tatizo likaisha mara moja? Marafiki zangu, hasa wale ambao ndiyo kwanza mmeingia kwenye ndoa hivi karibuni, lazima mjitahidi kutofautisha maisha ya ndoa na yale ya urafiki na uchumba.

 

KWANINI HASA?

Sababu za msingi zaidi nimezieleza hapo juu. Lakini jambo kubwa la kuongezea hapa ni kwamba, mnapokuwa kwenye ndoa, mnapaswa kufahamu kuwa mmejiunganisha kwa ajili ya maisha yenu moja kwa moja.

Wakati fulani mume anaweza kuwa bize  akihangaika na kufikiria kufanya kazi pengine zaidi ya tatu kwa wakati mmoja ili familia yake ijiendeshe sawasawa. Si rahisi muda wote kukawa na mahaba yale yaliyokuwa zamani.

Sawa, ni vyema kutenga muda wa kukaa na mwenzako na kufurahia maisha. Hapo mnaweza kuamua kutoka au pengine hata kama ni mazingira yaleyale lakini kwa staili tofauti na siku nyingine.

Kikubwa ni kuwekeza upendo wako wa dhati moyoni mwako na ujihakikishie kuwa uliridhika naye kabla ya kuingia kwenye muunganiko huo. Upendo ndiyo umebeba kila kitu.

 

MAHITAJI

Baadhi ya wanandoa (hasa wanawake) wamekuwa na tabia ya kuwalalamikia waume zao kuwa hawawapatii mahitaji yote ya muhimu kama zamani. Utakuta mwanamke anataka nguo mpya kwa mfano, anataka kupelekwa ufukweni au kwenye bendi.

Hayo ni mambo ambayo mumewe alikuwa akiyafanya wakati wa uchumba wao lakini sasa amebadilika. Jambo la kujiuliza, ni je, kuna tofauti ya tabia kati ya wakati huo na sasa?

Je, muda ambao umekuwa ukienda naye kwenye bendi ndiyo anaoutumia huko nje sasa hivi? Lakini nje inategemea na mahali anapokuwa. Mathalani yupo kwenye mihangaiko ya kutafuta fedha, si kosa.

Kumbuka sasa mpo kwenye ndoa, starehe si muhimu sana kama kujali familia na kutatua matatizo kwa haraka.

Siyo sawa kulalamika kwa kutotimiza baadhi ya mambo. Rafiki yangu, hataweza kufanya kila kitu, lakini pia kushindwa huko kusiondoe mapenzi ambayo yamejengeka moyoni mwako. Mpo kwenye mpambano wa maisha.

Wiki ijayo nitahitimisha mada hii, USIKOSE!

Je, ungependa kujiunga katika group letu la LOVE MOMENT katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp? Kama ndivyo andika ujumbe inbox ya namba yangu hapo juu, tutakunganisha ukutane na marafiki wengi na ujifunze zaidi kuhusu uhusiano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles