Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
FAINALI ya Michuano ya Kombe la Azam, inatarajia kufanyika leo kwa timu ya Azam kukabiliana na Lipuli FC, katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.
Azam FC waliingia hatua ya fainali baada ya kuifunga KMC bao 1-0 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Wakati wapinzani wao Lipuli FC waliingia hatua hiyo baada ya kuifunga Yanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Samora, Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na Azam FC kuhitaji ubingwa ili wapate fursa ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani baada ya kukaa kwa muda mrefu bila ya kupata nafasi hiyo.
Timu hiyo itashuka dimbani ikiwa na morali ya juu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Taifa jijini hapa.
Wanalambalamba hao wataivaa Lipuli wakiwa na nguvu zaidi kutokana na baadhi ya wachezaji wao waliokuwa majeruhi hali zao kuimarika.
Upande wao Lipuli watakuwa wakihitaji kuandika historia kwa mara ya kwanza ya kutaka kutwaa ubingwa huo ili wapate fursa ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Timu hiyo ambayo ilipanda daraja katika msimu wa mwaka 2017/18, imekuwa ikionyesha ushindani mkubwa hasa katika timu kongwe imepania kuendeleza ubabe kama walivyofanya katika mchezo wao dhidi ya Yanga.
Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limemtangaza Hance Mabena, kutoka Tanga kuwa mwamuzi wa mchezo huo.
Katika mchezo huo watatumika waamuzi sita kwa mara ya kwanza kwenye historia ya soka Tanzania ambapo Mabena atasaidiwa na jumla ya waamuzi watano (wawili wa pembeni, wawili kwenye magoli na mwamuzi mmoja wa akiba).
Taarifa ya TFF iliyotolewa jana, Mabena, atasaidiwa na Mohamed Mkono kutoka Tanga kama mwamuzi msaidizi namba moja, Ferdinand Chacha kutoka Mwanza kama mwamuzi msaidizi namba 2, Abubakar Mturo kutoka Mtwara atakuwa ni mwamuzi wa akiba.
Akizungumzia mchezo huo kocha mkuu wa Azam FC, Abdul Mingange, alisema anawaheshimu Lipuli FC kwani hawakufika hapo kwa kubahatisha hivyo lazima wawe makini.
“Tumejiandaa vya kutosha kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo huu, ukizingatia ni muda mrefu timu yetu haijashiriki michuano ya kimataifa,” alisema.
Kocha msaidizi wa Lipuli FC, Selemani Matola, alisema licha ya Azam FC kuwa ni timu nzuri hiyo haiwatishi kwani waliingia hatua hiyo kwa kuifunga klabu kubwa.
“Tumefanya maandalizi mazuri hivyo tutatumia udhaifu wa wapinzani wetu Azam FC kuhakikisha tunapata ubingwa na kutwaa kombe hili na kuandika historia kwenye timu yetu,” alisema.