Na HERIETH FAUSTINE
KOMAMANGA ni moja ya tunda lenye ladha nzuri na hupatikana zaidi katika maeneo ya Afrika Mashariki. Inasemekana kuwa tunda hili ni dawa nzuri kwa magonjwa mengi.
Komamanga hustawi katika miezi ya Septemba na Februari. Hushamiri zaidi kipindi cha joto, pia humudu hali ya ukame.
Komamanga si tunda tu bali ni chakula kilichojawa na afya ya vitamin, madini pamoja na virutubisho vingine vingi vinavyoweza kufanya mwili kuwa na afya na nguvu tele.
Juisi ya majani mabichi na machanga ya mmea huo hutibu magonjwa mbalimbali ikiwamo kuharisha damu.
Magome ya mti huo yanapochemshwa na kunywewa husaidia kutibu malaria na vidonda vya koo.
Wagonjwa wa saratani wanashauriwa kunywa juisi ya mbegu za mkomamanga, pia husaidia mtiririko wa damu kwenda vizuri katika mishipa ya damu hivyo kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kiharusi.
Hulinda meno na kuzuia kuoza, pia husaidia mfumo wa kinga ya mwilini kwa kuondoa vijidudu vya bakteria na maambukizi ya virusi ndani ya mwili. Mkomamanga husaidia kutibu pumu, matatizo ya njia ya mkojo, kuweka sawa mfumo wa chakula pamoja na kutibu ini na njia ya usagaji wa chakula.
Rojo rojo za mbegu ya mkomamanga ikichanganywa na maziwa, hutibu tatizo la mawe kwenye figo (Kidney Stone).
Komamanga pia ni mahiri katika kutibu tezi dume, kisukari, baridi yabisi na uvimbe katika maungio ya vidole.
Majani ya mkomamanga hutumika kutibu hali ya tumbo kujaa gesi na kudhibiti tindikali (acid) tumboni.