30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

MAZOEZI YA ASUBUHI NI BORA ZAIDI YA JIONI 

Dk. Fredirick L. Mashili, MD, PhD.


YAKO majadiliano ya muda mrefu kuhusu utofauti wa kufanya mazoezi asubuhi na jioni. Wengi wamekuwa wakijiuliza ni wakati gani ulio mzuri zaidi kwa kufanya mazoezi na kupata faida za kiafya zinazotokana na mazoezi hayo.
 
Hapa tunajadili sababu za kisayansi, kijamii na kimazingira zitakazokusaidia kukupa mwelekeo na kuweza kuamua ni muda gani ulio bora zaidi.
 
Sababu za kisayansi Vichocheo/homoni muhimu kama testosterone ambazo husaidia kukupa nguvu na hamu ya kufanya kazi huwa katika damu kwa kiasi kikubwa wakati wa asubuhi – hivyo, kukupa nguvu, uwezo na hamu ya kufanya mazoezi. Hali kadhalika testosterone husaidia kujenga misuli na kuchoma mafuta, mojawapo ya nia ya kufanya mazoezi.
 
Mazoezi pia husaidia kuongeza kiwango cha kemikali au vichocheo viitwavyo endorphins – maarufu vichochea furaha. Endorphins hutufanya kujisikia raha na kuwa wenye furaha. Ukifanya mazoezi wakati wa asubuhi kiwango cha endorphins kitaongezeka katika damu na mwili wako, hivyo kukufanya mwenye furaha siku nzima – kitu ambacho kitakusaidia kufanya shughuli zako vizuri.
 
Sababu za kijamii, mazingira na maisha 
Ziko nyingi. Ila muhimu ni ukweli kwamba ni rahisi kufanya mazoezi kuwa tabia, kama utayapangia muda wa asubuhi. Mambo mengi hujitokeza wakati wa jioni na kuharibu kabisa ratiba za mazoezi. Ni ukweli pia kwamba kutokana na kazi na mihangaiko ya siku, wengi wetu huwa tunakuwa tumechoka wakati wa jioni. Tafiti zinaonyesha kwamba, watu wanaofanya mazoezi wakati wa asubuhi hutimiza malengo yao haraka na mara nyingi zaidi ukilinganisha na wale wanaofanya mazoezi hayo wakati wa jioni.
Utafiti uliofanywa mwaka 2011 nchini Uingereza, unatoa mfano mzuri wa faida za mazoezi ya asubuhi ukilinganisha na yale ya jioni. Utafiti huu uliwahusisha wanawake 12 wenye afya bora, wenye wastani wa umri wa miaka 25, na ambao hawakuwahi kufanya mazoezi hapo awali. Wanawake hawa waligawanywa katika makundi mawili, ambapo kundi moja lilifanya mazoezi wakati wa asubuhi na kundi linguine lilifanya mazoezi hayo hayo wakati wa jioni.
 
Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kwamba, miili ya wanawake waliokuwa wakifanya mazoezi wakati wa asubuhi ilikuwa ikitumia/kuchoma mafuta zaidi kuliko ile ya wale waliofanya mazoezi wakati wa jioni. Miili ya wanawake waliofanya mazoezi wakati wa asubuhi ilikuwa pia na uwezo wa kutumia zaidi chakula cha mafuta kilicholiwa baada ya mazoezi –ikimaanisha kuongezeka kwa uwezo wa kuchoma mafuta. Utafiti huu ulihitimisha kwamba, mazoezi ya asubuhi yanafaida zaidi kiafya ukilinganisha na yale yanayofanywa wakati wa jioni, kutokana na miili kuwa na uwezo wa kuchoma mafuta zaidi pale mazoezi yanapofanywa wakati wa asubuhi.
 
Japo kuna tafiti zingine zinazoonyesha faida zaidi kwa kufanya mazoezi jioni, lakini kwa ujumla ukijumlisha sababu za kisayansi na zile za kimaisha na kimazingira –kufanya mazoezi asubuhi huenda kukakupatia matokeo mazuri zaidi kiafya.

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana naye kwa namba 0752255949, barua pepe, [email protected] Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.or

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles