Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Timu ya Fountain Gate Academy inayoshiriki Ligi daraja la kwanza imemtambulisha, Denis Kitambi kuwa Kocha Mkuu kwa kandarasi ya mwaka mmoja.
Kitambi ambaye amewahi kuwa Kocha Msaidizi wa timu za Simba SC, Azam Fc, Ndanda Fc na FC Leopards ya Kenya anachukua nafasi ya Mohammed Muya ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo.
Akizungumza leo, Alhamisi June 16,2021, Mkurugenzi wa Fountain Gate Academy, Japhet Makau amesema Kitambi ataiongoza timu msimu ujao wa Ligi daraja la kwanza.
“Tumeingia makubaliano na Denis Kitambi awe Kocha Mkuu wa timu yetu, ni Mwalimu mwenye uzoefu Msaidizi wake atakuwa, Mwalimu Robert Bagio lakini pia tutakuwa na mchambuzi wa mechi (Match Anaysis) analisis ambaye atatusaidia timu yetu kujiendesha kiweledi,”amesema.
Kwa upande wake, Kitambi amesema anashukuru kufanya kazi na Fountain Gate kutokana na kujiendesha kiweledi. Amesema usajili atakaufanya ni wachezaji wenye uzoefu pamoja na damu changa.
Kitambi amesema timu yake soka la kushambilia huku akikiri ligi daraja la kwanza inahitaji kujiandaa vyema kimbinu.
“Sasa naanza kusajili nitakuwa na wiki nane, kikubwa naomba ushirikiano kutoka kwa mashabiki na uongozi wa timu,”amesema.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo ametangaza timu hiyo itatumia Uwanja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Gairo kama uwanja wake wa nyumbani na rasmi imehama mkoani Dodoma.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Gairo, Winfrid Mponela amesema uwepo wa timu hiyo,Wilayani Gairo utafungua milango ya vipaji vya Wilaya hiyo kuonekana.