Winfrida Mtoi, Dar es Salaam
KAMATI ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, imempa onyo kali Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck kutokana na kitendo cha kugoma kuwafungulia mlango waamuzi na kamishina wa mechi wakati wa ukaguzi.
Tukio hilo lilitokea Februari Mosi, mwaka huu wakati wa mchezo wa Simba na Coastal Union uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana, adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni namba 41(13) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa makocha, ikiwa ni uamuzi wa kikao kilichofanyika Februari 10, 2020.
Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, Ofisa Mhamasishaji wa timu hiyo, Antonio Nugaz, Kocha wa Namungo FC, Hitimana Thiery na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, wamepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Pia kikao hicho kimeilekeza sekretarieti kufuatilia viongozi wa klabu na makocha ambao hivi karibuni wamekuwa wakishutumu na kutoa matamshi yenye kukashifu na kudhalilisha viongozi na chapa ya ligi hiyo na taasisi kwa ujumla.
“Viongozi na makocha waliobainika kutoa shutuma hizo ni wa Namungo FC, Hitimana Thiery katika mchezo wa Simba na Namungo, Luc Eymael kwenye mchezo wa Yanga na Lipuli, huku wengine ni Manara na Nugaz,” ilisema taarifa hiyo.
Nayo klabu ya Polisi Tanzania imepigwa faini ya Tsh. 1,500,000 kwa kosa la kutumia mlango usio rasmi wa kuingia uwanjani katika mechi yao na Simba iliyochezwa Februari 04, 2020 Uwanja wa Taifa.
Adhabu nyingine imemkumba mwamuzi Abubakar Mturo, aliyefungiwa kwa miezi mitatu kwa kosa la kushindwa kumudu mchezo kati ya mechi iliyochezwa Februari 05, 2020 katika uwanja wa Taifa, Yanga ilipocheza na Lipuli.
Nahodha wa Azam FC, Aggrey Morris yeye amepigwa faini ya Tsh 200,000 kwa kosa la kugoma kuzungumza na waandishi wa habari katika mchezo wao wa Februari 5, dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.