31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Kocha Etoile aingia mitini

faouzibenzartiNA ONESMO KAPINGA

KOCHA Mkuu wa Etoile du Sahel ya Tunisia, Faouzi Benzarti, ameingia mitini baada ya kushindwa kutokea katika mkutano wa makocha na waandishi wa habari ulioandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa leo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Benzarti alishindwa kuhudhuria mkutano huo kwa madai walichoka baada ya kuwa angani kwa saa tisa wakitokea Tunisia ambapo waliwasili Dar es Salaam jana alfajiri.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, Benzarti aliwataarifu kwamba asingefika kwenye mkutano huo na kuwaomba radhi kutokana na hilo.

Pamoja na kushindwa kutokea kwa kocha huyo, Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema amezikamata mbinu za Etoile du Sahel na atahakikisha wanashinda mchezo huo wa raundi ya pili wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo huo utakaoanza 9:00 alasiri, Pluijm alisema amejiandaa kikamilifu katika kuhakikisha wanashinda nyumbani ili waweze kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele watakaporudiana ugenini Mei Mosi, mwaka huu.
Alisema anafahamu mbinu za wapinzani wao ambao mara nyingi wanapokuwa ugenini wanafanya mashambulizi ya kushtukiza, huku wakilinda lango lao ili wasifungwe mabao mengi.
Alisema atahakikisha wachezaji wake wanatibua mipango yao kwa kuwalazimisha kufuata mfumo watakaocheza wao ili kuleta uwiano wa soka.
Alisema Eitole ni kati ya timu bora Afrika, lakini wataingia kwenye vita na kushinda, hivyo mashabiki wanatakiwa kufika kwa wingi kuishangilia timu yao.
Pluijm amewataka wachezaji wake kutofanya makosa ambayo yaliwasababishia wang’olewe mapema na Al Ahly ya Misri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.
Alisema wachezaji wake walishindwa kuzitumia nafasi zaidi ya tano za kufunga katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, ambao walitolewa kwa penalti 4-3 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 mjini Alexandria.
Pluijm alisema kwa kulitambua hilo wachezaji wake hawatorudia makosa kwani wanatakiwa kushinda kwa idadi kubwa ya mabao ambayo yatakuwa ni mtaji kwao katika mchezo wa marudiano.
Alisema anaiheshimu Etoile du Sahel lakini wachezaji wake wamempa matumaini ya kushinda, kutokana na nidhamu waliyoionyesha katika mazoezi akiamini lolote linaweza kutokea ndani ya dakika tisini.
Alisema amewaandaa wachezaji wake kiufundi na kisaikolojia waweze kujiamini na kupata matokeo mazuri katika uwanja wao wa nyumbani.
Katika mchezo huo, Pluijm anaweza kuwakosa Amisi Tambwe ambaye anaugua malaria na Salum Telela aliyeumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, uliochezwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga kinachotarajia kushuka uwanjani leo ni Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Mrisho Ngassa, Kpah Sherman na Haruna Niyonzima.
Yanga wakiwatoa Etoile du Sahel wataingia katika hatua ya mtoano wakiisubiri timu ambayo itashindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles