Na Winfrida Mtoi
UONGOZI wa Klabu ya KMC umempa mkataba mpya wa mwaka mmoja beki wake Andrew Vincent ‘Dante’, kuendelea kutumikia kikosi hicho katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/2022.
Dante alijiunga na KMC msimu uliopita akitokea Yanga na ameonesha kiwango kizuri akijihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Mchezaji mwingine aliyeongezewa mkataba na KMC ni kiungo Jean Baptiste Mungiraneza, raia wa Rwanda.
Katika kuboresha kikosi chake, timu hiyo ya Manspaa ya Kinondoni, imekamilisha usajili wa wachezaji kadhaa waliotamba msimu uliopita akiwamo kipa Farouk Shikalo aliyekuwa Yanga, Hassan Kessy akitokea Mtibwa Sugar na Mohammed Kassim kutoka Polisi Tanzania.