24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Klopp: Sijawahi kupata kichapo kama hiki

BIRMINGHAM, ENGLAND

KOCHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Liverpool, Jurgen Klopp, ameweka wazi kuwa, hajawahi kupata kichapo kikubwa kama alichopata juzi dhidi ya Aston Villa cha mabao 7-2.

Klopp amesema, tangu ajiunge na klabu hiyo 2015, amepoteza michezo mbalimbali lakini haijawahi kutokea kufungwa mabao mengi kama ilivyotekea juzi.

Hata hivyo, Aston Villa wameandika historia mpya ya kuwa klabu ya kwanza kuifunga Liverpool mabao saba tangu walipofanya hivyo Tottenham mwaka 1963.

Kwa upande mwingine, Liverpool wameandika historia ya kuwa klabu ya kwanza kama bingwa mtetezi kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao kwenye michezo ya awali mara baada ya timu ya Arsenal kufanya hivyo mwaka 1953.

“Kwa sababu mbalimbali naweza kusema Aston Villa walikuwa vizuri sana, waliweza kulazimisha kutumia vizuri makosa yetu. Mchezo ulikuwa wa wazi kabisa, lakini ukweli ni kwamba tulitengeneza makosa mengi.

“Kila wakati Aston Villa walikuwa wanafanikiwa kuupata mpira, waliweza kupiga mipira mirefu, lakini kwa upande wetu tulishindwa kuwazuia na kupokonya mipira.

“Kitu cha kushangaza ni kwamba, vitu ambavyo havitakiwi kufanyika kwenye soka sisi tukawa tunavifanya, hivyo nitumie nafasi hii kuwapongeza wapinzani Aston Villa, hatukutegemea matokeo kama haya, lakini ndivyo ilivyotokea, lazima nikubaliane kuwa ni matokeo mabaya kuwahi kutokea kwa upande wangu,” alisema Klopp.

Kwenye mchezo huo, Liverpool walishuka dimbani bila ya mlinda mlango wao namba moja Alisson Becker ambaye anasumbuliwa na tatizo la bega, hivyo mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita. Nafasi ya kipa huyo ilizibwa na Adrian ambaye aliruhusu mabao matatu kutoka kwa mshambuliaji mpya wa Aston Villa, Ollie Watkins.

Mabao mengine ya Aston Villa yalifungwa na Jack Grealish akipachika mawili, huku Ross Barkley na John McGinn wakifunga bao moja moja, wakati huo mabao ya Liverpool yakifungwa na Mohamed Salah.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles