25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kizimbani kwa kutakatisha Sh bilioni 31.57 za kodi ya vileo

Kulwa Mzee – Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Kampuni ya Jaruma General Supplies Ltd, Lucas Mallya na wenzake nane, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 28 ya uhujumu uchumi, ikiwamo kukwepa kodi, kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 31.57 na kutakatisha fedha hizo.

Washtakiwa hao walifikishwa jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Faraja Nguka.

Mbali na Mallya, washatakiwa wengine ni Emmanuel Peter, Happy Mwamugunda, Prochesi Shayo, Prokolini Shayo, Geofrey Urio, Nyasulu Nkyapi, Tunsubilege Mateni na Nelson Kahangwa.

Akisoma mashtaka, Wakili Nguka alidai katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Januari 2015 na Januari 7, 2020 jijini Dar es Salaam kwa pamoja waliongoza genge la uhalifu kwa nia ya kupata faida.

Alidai shtaka la pili hadi la saba yanamkabili Lucas ambaye anadaiwa Juni 3, 2019 Dar es Salaam alighushi, kutengeneza stempu ya ushuru akionyesha imetengenezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati si kweli.

Lucas anadaiwa alitoa nyaraka hiyo ya kughushi TRA akionyesha ni halali wakati akijua si kweli.

Katika shtaka linguine, inadaiwa Januari 7 mwaka huu, Chang’ombe A, Temeke, Dar ea Salaam alikutwa na rola 93 za stempu zenye thamani ya Sh 80,516,000 alizochapisha bila kibali cha Kamishna wa Mapato.

Lucas anadaiwa kati ya Januari 2016 na Desemba 31, 2019 Dar es Salaam, kwa kutengeneza stempu hizo za kughushi, alisababisha hasara kwa Serikali ya Sh 15,241,075,169, akikwepa kodi kiasi hicho cha fedha.

Shtaka la saba anadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zinatokana na zao la kukweka kodi.

Akisaidia kusoma mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Zackaria Ndaskoi alidai mshtakiwa Emmanuel anadaiwa Januari 3 mwaka huu, Mbezi Makabe alikutwa na rola za stempu zenye thamani ya Sh 1,104,000 zilizochapishwa bila kibali cha Kamishna wa Kodi.

Shtaka la tisa linamkabili Happy Mwamugunda ambaye ni Mkurugenzi wa Happy Imports Associates, anayedaiwa Januari 2017 na Desemba 2019 bila kusajiliwa na kamishna wa kodi aliingiza katoni 413 za Drostdy Wine zenye thamani ya Sh 24,780,000 na shtaka la 10 anadaiwa kukwepa kodi ya Sh 9,584,401,393.

Mshtakiwa huyo anadaiwa katika kipindi hicho alisababisha hasara ya Sh 9,584,401,393 na kutakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua fedha hizo zinatokana na zao la kukwepa kodi.

Shtaka la 13 linawakabili Proches na Prokolini ambao wanadaiwa Desemba 2019 walisambaza bidhaa zilizowekwa stempu za kughushi, katoni 749 za Wine 75CL zenye thamani ya Sh 98,670,000, katoni 594 za Drostdy hof 37.5CL zenye thamani ya Sh 12,002,000, katoni 14 za Cousins 75CL14 zenye thamani ya Sh 16,240,000 na katoni za Amalula 58 zenye thamani ya Sh 12,120,000 ambapo zote thamani yake Sh 139,032,000.

Washtakiwa hao wanadaiwa katika shtaka la 14, walikwepa kulipa kodi Sh 38,827,276, shtaka la 15 walikwepa kulipa kodi Sh 2,359,342,542.07 na shtaka la 16 na 17 wanadaiwa kusababisha hasara ya jumla ya fedha hizo.

Wakili Zackaria alidai shtaka la 18 linamkabili Urio ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya GMU group, anayedaiwa Desemba 2018 kwa nia ya kukwepa kodi, aliwasilisha taarifa za hesabu za uongo TRA na kusababisha kukwepa kodi ya Sh 4,265,882,773.

Mshtakiwa huyo anadaiwa katika shtaka la 19 na 20 kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha na kutakatisha fedha hizo, huku akijua zinatokana na zao la kukwepa kodi.

Shtaka 21 linawakabili Mateni na Kahangwa, wanaodaiwa kati ya Januari 2015 na Desemba 31, 2018 wakiwa mhasibu na mkaguzi wa hesabu walitengeneza taarifa za uongo za mwaka 2015, 2016 na 2017 kwa nia ya kupata faida.

Katika shtaka la 22, washtakiwa wanadaiwa kumsaidia Urio kuandaa hesabu za uongo za miaka hiyo kwa nia ya kujipatia faida na shtaka la 23 ,wanadaiwa kutakatisha Sh 4,265,882,773.

Shtaka la 24 mshtakiwa Nkyapi anadaiwa kushindwa kulipa kodi ya Sh 89,673,373 na katika shtaka la 25, anadaiwa baada ya kupokea malipo ya Sh 98,670,000 ya wine aina ya  Robertson alishindwa kutoa risiti ya kielektroniki.

Katika shtaka 26, 27 na 28 mshtakiwa Nkyapi anadaiwa kuingiza vinywaji vikali bila kusajiliwa vyenye thamani ya Sh 95,100,297, anadaiwa kusababisha hasara ya Sh 89,673,337 na anadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote, upelelezi haijakamilika na kesi iliahirishwa hadi Februari 12 mwaka huu. Washtakiwa wanatetewa na mawakili mbalimbali akiwemo Hudson Ndusyepo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles