24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Afungwa jela maisha kwa kulawiti mtoto wa miaka minane

Kulwa Mzee – Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, imemuhukumu mkazi wa Gongo la mboto, Stambuli Yusufu (35), kifungo cha maisha jela kwa kumwingilia kinyume na maumbile mtoto wa miaka 8.

Alitiwa hatiani jana mbele ya Hakimu Mkazi, Jimson Mwankenja.

Yusufu ameamriwa kulipa fidia ya Sh milioni mbili na akishindwa kulipa apigwe viboko 12 ndipo aanze kutumikia kifungo chake cha maisha jela.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kumfanyia kitendo hicho, mtoto huyo ambaye alikuwa akisoma darasa la nne, kati ya mwaka 2017 na 2018.

Katika ushahidi, inadaiwa baada ya tendo hilo, mshtakiwa alikuwa akimpa mtoto huyo Sh 1,000 hadi Sh 2,000 kisha anamtishia iwapo atamwambia mtu atamuua.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwankenja alisema kifungo hicho cha maisha jela kitaanza kuhesabiwa  baada ya mshtakiwa kumlipa Sh milioni mbili mtoto huyo.

“Endapo mshtakiwa atashindwa kulipa fidia hiyo, basi apigwe viboko 12 ndipo aanze kutumikia kifungo chake cha maisha jela.

“Mahakama imezingatia ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka, utetezi wa mshtakiwa mwenyewe na uzito wa kosa hilo husika,” alisema Hakimu Mwankenja.

Aliongeza kuwa mahakama imezingatia masilahi ya jamii, mshtakiwa mwenyewe na busara za Bunge kupitia kifungu cha sheria cha 154(1) na (2) na kutoa adhabu  hizo ili iwe funzo kwa watu wote wenye tabia kama hiyo.

Hakimu Mwankenja aliwataka mawakili wa upande wa mashtaka kuwajibika vema kwa kuoanisha vifungu vya sheria kwa ufasaha kwenye hati za mashtaka.

“Katika kesi hii, kwenye hati ya mashtaka kiliandikwa kifungu cha 154(1) na (2) bila ya kuainisha kama kilifanyiwa marekebisho na kifungu cha 16 cha makosa ya kujamiiana namba 4 ya 1998 na kwamba hiyo ilikuwa ni shida.

“Katika kesi hii, kosa hilo lilitibika kwa sababu mshtakiwa alikuwa anaelewa anashtakiwa kwa kosa gani na kwamba mapungufu hayo yalirekebishika kwa mujibu wa kifungu cha 388 cha mwenendo wa mashauri ya jinai,” alisema Hakimu Mwankenja.

Wakili wa Serikali, Nancy Mshumbusi kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, aliieleza mahakama kuwa hana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshtakiwa na kwamba ni mkosaji wa mara ya kwanza.

Aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa mtoto ana miaka 8 na amefanyiwa kitendo hicho kati ya mwaka 2017 na 2018.

Kwa upande wake, mshtakiwa aliiomba mahakama impatie adhabu ndogo kwa kuwa ana familia inayomtegemea na ni mkosaji wa mara ya kwanza.

Awali Stambuli aliposomewa shtaka hilo alikana na upande wa mashtaka uliita mashahidi sita; mwalimu, mama mzazi wa mtoto huyo, askari polisi, daktari wa hospitali ya Mnazi Mmoja na kiongozi wa Serikali ya Mtaa katika eneo wanaloishi ambao kwa nyakati tofauti walitoa ushahidi wao.

Wakati wa utetezi, Stambuli alidai Agosti 8, 2018 alivamiwa na kikundi cha watu akituhumiwa kuwa anatoa mafunzo kwenye kikundi cha Panya Road.

Alidai walimkamata na kumpeleka Kituo cha Polisi Gongo la mboto na baadaye alipelekwa Kituo cha Polisi Stakishari na hatimaye mahakamani, na kwamba hicho ndicho anachokifahamu, hivyo kesi ya kulawiti alibambikiwa.

Hakimu Mwankenja akichambua hukumu hiyo, alisema mapungufu yaliyojitokeza wakati wa usikilizwaji wa kesi ya upande wa mashtaka ni mama mzazi wa mtoto na mwalimu ambao ushahidi wao ulikuwa ni wa kusimuliwa, hivyo haukuwa na nguvu.

Kwa upande wa ushahidi wa askari na kiongozi wa Serikali ya mtaa, nao ulikuwa na mapungufu kwa sababu hakuna aliyeshuhudia tukio la mtoto huyo kulawitiwa, hivyo haukuwa na mashiko.

“Mahakama haikuridhishwa na kitendo cha mama mzazi wa mtoto kuomba fomu ya PF3 ipokelewe mahakamani kama kielelezo, kwa sababu haukuwa utaratibu, ilipaswa kutolewa na mtendewa ambaye ni mtoto ama daktari.

“Hata pasipokuwepo na ushahidi wa kimatibabu, kesi ya upande wa mashtaka haiwezi kufa endapo tu kuna ushahidi mwingine ambao unaweza kumtia hatiani na kumpa adhabu, kesi itaendelea kusimama.

“Katika makosa ya kubaka na kulawiti, ni lazima ithibitike ni kweli mtendewa aliingiliwa kwenye sehemu yake ya nyuma,” alisema Hakimu Mwankenja.

Alisema mahakama ilijikita katika ushahidi wa mtoto na daktari ambao ulimfanya mshtakiwa kutiwa hatiani.

Hakimu Mwankenja alisema mahakama ilichukua tahadhari kwa kuzingatia matakwa ya sheria na kujiridhisha kuwa mtoto anasema ukweli, anajua nini maana ya kiapo, ana uelewa na ni kweli aliingiliwa kwenye sehemu zake za nyuma na aliyemwingilia ni mshtakiwa.

Mtoto alieleza kuwa anamfahamu mshtakiwa huyo, anakaa karibu na shule na ushahidi wake uliungwa mkono na daktari kuwa ni kweli aliingiliwa.

Alidai anafahamu chumbani kwa mshtakiwa huyo na kwamba alimpa maagizo avue chupi yake kisha akamwingizia uume wake sehemu ya haja kubwa.

Mtoto huyo katika ushahidi wake, alidai alisikia maumivu sana wakati mshtakiwa akifanya kitendo hicho na alikuwa akipewa Sh 1,000 hadi 2,000 na kuambiwa asiseme lolote nje vinginevyo atamuua.

Kwenye ushahidi wake, mtoto huyo alidai alishindwa kuwaeleza wazazi kwa sababu aliogopa atauawa kama alivyoahidiwa na alifanyiwa vitendo hivyo mwaka 2017 hadi 2018.

Ushahidi huo uliifanya mahakama iridhike kuwa kosa limethibitika pasipo kuacha shaka na mshtakiwa alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles