Na RAMADHANI MASENGA
BAADA ya Steven Charles Kanumba kufariki, kila mpeda filamu alijua ilikuwa ni fursa ya Ray kulifanya soko namna anavyopenda.
Wakati wa uhai wa Kanumba, mshindani wake wa karibu alikuwa Ray. Kwanini sasa watu wasingeamini kuwa baada ya mmoja kuondoka aliyebaki ndiye angekuwa mfalme asiyepingika?
Ila bahati mbaya sana haikuwa hivyo. Ray kalala. Aliyeshika sokoni baada ya kifo cha Kanumba alikuwa Jacob Stephen ‘JB’. Yeye akawa kila kitu katika soko la filamu.
Alitoa filamu mchana ikatamba na akatoa nyingine jioni ikafunika ile ya mchana. Watoto mtaani wakaanza kujifananisha naye.
Kila gazeti likawa na stori yake. Akajiita bonge la bwana na kila jina lililompendeza. Nani alipinga ufalme wake? Miezi michache upepo ukabadilika.
Watu wakaanza kumwelewa Gabo. Wakaona ana kitu cha ziada kuliko wengine. Wakamuweka pembeni JB na kuanzia kumfuatilia yeye.
Kila msanii chipukizi ungemuuliza nani anamkubali, wasingemtaja Jb tena. Wote walimsifia Gabo. Walimsifia kwa kila kitu.
Kuanzia kuigiza kwake mpaka maisha binafsi. Gabo alishika kila kona, makampuni ya matangazo nayo yakammiminikia. Nani hakuona kipaji chake?
Ila wakati Gabo anatamba kuna mtu alikuwa anatabiriwa japo hakufikia malengo. Huyu ni Rammy Gallis. Mbali na mwonekano wake na angalau uthubutu wake, Rammy hakuja na kitu kipya.
Walau Gabo alitaka kutupa mambo ambayo wengine walishindwa. Ila Gallis hapana. Watu walimfananisha na Kanumba. Ila ukweli hakuwa mbunifu kama marehemu Steve.
Kuna nini katika filamu? Udumavu wa flamu unachangiwa pia na usingizi waliolala kina Gallis na Gabo. Wakati katika Bongo Fleva, Juma Nature akiwa hana pumzi kama za mwanzo, Ali Kiba na Diamond wanakimbiza mpaka basi.
Hii ndiyo tofauti kati ya Bongo Fleva na Bongo Muvi. Katika Bongo Fleva, wasanii wa sasa wanafanya makubwa kuliko wasanii wa zamani, ila Bongo Muvi wasanii wa zamani walifanya makubwa kuliko wasanii wa sasa.
Gabo na Gallis wanatakiwa kuumiza vichwa zaidi. Kumtegemea JB kufanya makubwa ni dalili ya udumavu wa sanaa. Ndiyo kusema katika miaka yote, Bongo Muvi imeshindwa kuzalisha wasanii wengine wenye uwezo na weledi kama kina JB mpaka leo tuwe tunawategemea wao tu?
Sanaa ya sasa inamuhitahji mtu mjanja na mbunifu. Gabo na Gallis wana vipaji ila wanaonekana kushindwa kujua ni uchawi gani wawaroge Watanzania na kuwateka kama walivyowahi kutekwa na wengine.
Katika wakati huu ambao watu wanamchukulia Ray kama msanii mkongwe, Gabo na JB walibidi kutawala soko. Kwanza kutokana upya wao na pia kutokana na kudorora kwa kasi ya Ray na Jb.
Kwanini mpaka sasa wametulia tu? Au na wenyewe wamepatwa na ugonjwa wa kuamini mchawi wa sanaa yao ni series za Kikorea? Kama ndivyo, basi mgonjwa Bongo Muvi anaweza kufia mapokezi.
Nimeandika mara kadhaa kwamba mbaya wa Bongo Muvi sio sinema za kihindi wala Tamthilia za Kikorea. Tatizo la wao wenyewe.
Wao hawataki tena kuwa wabunifu na kujua nini Watanzania wanataka na kuishia kufanya kazi kwa mazoea. Kwa mtindo huu ni lini utateka tena watu katika zama hizi za mitandoa ya kijamii?
Kwa ujana wao na upya wao Gabo na Rammy Gallis wanafaa kuwa wasanii wakubwa mara kumi ya namna walivyo leo.
Wajiulize wanakosea wapi? Wajifunze ni kitu gani kipya wakifanya Watanzania watafurahia na kuutukuza uwezo wao.
Kufanya makubwa katika sanaa hakuji kwa bahati mbaya. Inabidi kujitoa na kujitesa. Kina Gabo kama kweli wanataka kufanya makubwa zaidi hawatakiwi kujiona mastaa.
Wanatakiwa kujijua wana deni kubwa waliloachiwa na waliotangulia kuifikisha sanaa ya uigizaji hapa ilipo.