GWIJI wa Arsenal, Thierry Henry anaamini Santi Cazorla amekuwa ‘mtaamu’ sana uwanjani na kiwango chake ndicho kilichangia timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Manchester City katika mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa Etihad juzi.
Akizungumza katika mechi yake ya kwanza kama mchambuzi wa soka wa kituo cha televisheni cha Skysport, Henry alidai Cazorla ndiye alikuwa msingi wa kiwango bora kilichoonyeshwa na Arsenal katika mechi hiyo.
Cazorla alifunga bao la kuongeza kwenye kipindi cha kwanza kwa njia ya penalty kabla ya kumpigia pande safi, Olivier Giroud, ambaye alipiga bao la pili kwenye mchezo huo ambao ulikuwa wa kwanza kwa City kupigwa bao mbili au zaidi tangu mwaka 2010.
Baada ya mchezo huo, Henry alimmwagia sifa kibao Cazorla huku akisisitiza kuwa Mhispaniola huyo ndiye msingi wa kufufuka upya kwa Arsenal msimu huu.
“Alitawala kiungo. Kuonyesha kiwango kama hiki hapa Etihad ni kitu cha kipekee,” alisema Henry.
“Mchezaji wa kipekee sana. Nilisema kabla ya mechi kwamba watu wanamtolea macho Sanchez (Alexis), lakini kwa sasa Cazorla ndiyo mtua mbaye anaifanya Arsenal icheze. Sanchez hakuwa na kiwango kizuri leo, lakini wameshinda 2-0.
“Umeona lini mara ya mwisho Man City inashindwa kutengeneza hata nafasi moja ya kufunga? Najua walipiga mashuti kadhaa lakini hawakutengeneza nafasi yoyote ya maana.
“Siku zote anatabasamu (Cazorla). Pia nilipenda kuona akijaribu kuwatuliza wenzake pale timu ilipokuwa inashambuliwa.
“Ni muhimu sana kwake kucheza katikati. Inakuwa tofauti sana akicheza pembeni. Sidhani kama ana mwili au nguvu za kupambana pembeni. Unapocheza katikati unakuwa karibu na kila mtu, anaweza kufanya awezalo usiku kucha.”
Kiwango cha Cazorla kiliisaidia Arsenal kushinda kwa mara ya kwanza ugenini dhidi ya timu zilizo nne bora tangu Oktoba 2011 pale Robin van Persie, alipopiga hat-trick na kuipa timu hiyo ushindi wa mabao 5-3.