29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Kinachommaliza Owino Simba chatajwa

7NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
IMEELEZWA mvutano wa maslahi wa mara kwa mara kati ya wachezaji wa Simba SC na viongozi wao unachangia kushusha viwango vyao kutokana na kutumia muda mwingi kufuatilia haki zao badala ya kuendeleza vipaji vyao, jambo ambalo linadaiwa kummaliza beki Mganda, Joseph Owino.

Mwishoni mwa mwaka jana baadhi ya wachezaji wa kimataifa wa Simba waliujia juu uongozi wao na kutaka kulipwa stahiki zao kwa wakati, akiwemo beki mahiri Mganda, Owino, ambaye aligoma kuichezea timu hiyo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, huku uongozi ukidai ni mgonjwa.

Wachezaji wengine waliotishia kuikacha timu hiyo kwa madai ya kutolipwa stahiki zao ni wachezaji wapya Jjuuko Murshid na Simon Sserunkuma, ambao baadaye walikaa chini na uongozi na kumaliza tofauti zao.

Akizungumzia kiwango cha Owino, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba Mzambia, Patrick Phiri, alisema beki huyo ni miongoni mwa wachezaji bora wenye uwezo mkubwa katika soka kutokana na kiwango alichoonyesha wakati anakinoa kikosi hicho kabla ya kutimuliwa.

Alisema kiwango cha Owino kinashuka kutokana na mwenendo wake wa kutoroka mara kwa mara kwa madai ya kutofautiana na uongozi kuhusiana na maslahi yake ndani ya klabu hiyo.

“Kwa muda mfupi ambao niliifundisha Simba Owino alikuwa mmoja kati ya mabeki bora, lakini kwa mwenendo wake wa sasa uwezo wake unaweza kushuka kutokana na kushindwa kutuliza akili yake katika mpira na kuwaza mambo mengine,” alisema.

Alisema wachezaji wa kigeni ndio wanaongoza kwa utoro na kuomba ruhusa ambazo hazina msingi wowote kwa manufaa yao na timu, lakini kwa upande mwingine uongozi ndio unachangia kwa kiasi kikubwa jambo hilo kwa kushindwa kumalizana nao kwa wakati juu ya stahiki zao.

Kwa sasa kikosi cha Simba kinanolewa na kocha Mserbia, Goran Kopunovic, aliyeanza kazi rasmi Januari 7, mwaka huu, ambaye tayari amevutiwa na kiwango cha Jjuuko, anayecheza kama beki wa kati, jambo ambalo linaongeza ugumu kwa Owino kupata namba.

Baada ya Owino kukosa namba, kwa sasa Jjuuko anashirikiana na nahodha wa timu hiyo chipukizi, Hassan Isihaka, aliyeonekana kufanya vizuri kwenye beki ya kati kwa siku za hivi karibuni.

Phiri aliondolewa Simba baada ya timu hiyo kushindwa kutamba katika mechi nane za mzunguko wa kwanza Ligi Kuu kwa kupata matokeo ya sare sita mfululizo, kushinda na kufungwa mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles