27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kiwanda cha Sukari Kilombero kuanza mradi wa kuchochea ukuzaji uchumi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, ambacho kinamilikiwa na Kampuni ya Illovo Sugar Africa kwa Asilimia 75 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 25, kinatarajia kuanza mradi wake wa upanuzi ambao utakuza mchango wa kampuni hiyo katika ukuaji wa uchumi kutoka Sh bilioni 340 za sasa hadi kufikia takribani Sh bilioni 700 kwa mwaka.

Mradi huo wa upanuzi utakaohitaji uwekezaji mpya wa awali wa zaidi ya Sh bilioni 550, unajumuisha kiwanda kipya kitakachokuza uwezo wa kampuni hiyo wa kutengeneza sukari na kupunguza uhaba wa sukari nchini kupitia chapa yake ya “Bwana Sukari”.

Hii ni miongoni mwa mikakati ya kampuni hiyo katika kufikia maono yake ya kupunguza utegemezi wa nchi katika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kwa kuhakikisha kuwa inajitosheleza katika uzalishaji wa sukari ifikapo 2025.

“Mradi wetu wa upanuzi utakuza uzalishaji wa sukari kutoka tani 126,000 hadi tani 271,000 kwa mwaka hivyo kuisaidia Serikali kuokoa takribani dola milioni sabini za kigeni katika uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi,” anasema Ephraim Mafuru,

Mkuu wa Mauzo wa Illovo Sugar Africa, akizungumza katika Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha uliofanyika jijini Dodoma juzi.

Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu ya “Kuimarika kwa Uchumi wa Tanzania kutoka katika Janga la Uviko-19 na hali ya Baadaye” ulifanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre kuanzia tarehe 25 hadi 26 Novemba, 2021 na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Hassan Suluhu.

Mkutano huo ulilenga kuwakutanisha wadau ili kujadili ukuaji wa uchumi wakati na baada ya janga la Uviko-19, mijadala ikiangazia mchango wa maendeleo ya kidijitali, sarafu za kidijitali, pamoja na wajibu wa Serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi katika kufufua uchumi.

“Kampuni ya Sukari ya Kilombero imedhamiria kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua uchumi kutokana na janga la Uviko-19. Pamoja na kukuza mchango wetu katika ukuaji wa uchumi, upanuzi huo utazalisha fursa za ajira za kudumu 2,000 na ajira 2,440 za mikataba, pamoja na kuzalisha 10-15MW za umeme wa nishati mbadala zinazoweza kuingizwa kwenye gridi ya taifa kupitia Mkataba wa Ununuzi wa Umeme (Power purchase agreement – PPA) na TANESCO,” alisema.

Mafuru aliongeza kuwa upanuzi huo unatarajiwa kukuza kiwango cha miwa kinachonunuliwa kutoka kwa wakulima ifikapo 2026/27 kwa takribani tani milioni 1 kwa mwaka zaidi ya tani 600,000 zinazonunuliwa sasa na hivyo kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na uboreshaji zaidi wa miundombinu ya maendeleo na huduma za kijamii katika jamii zilizo jirani na Kiwanda cha Sukari cha Kilombero..

Ujio wa Uviko-19, kwa kiasi kikubwa, umeyumbisha ukuaji wa uchumi kote duniani. Kiwanda chetu kipya kitawezesha kwa kiasi kikubwa kuunga mkono mkakati wa serikali wa kufufua uchumi, haswa kupitia ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa viwanda. Ni dhamira yetu kuendelea kuchangia katika kuboresha maisha ya jamii zinazotuzunguka na kukuza uchumi wa nchi kwa kuongeza mapato ya wakulima, kuongeza mapato ya serikali, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, sambamba na kujenga thamani ya muda mrefu kwa wadau wetu wote,” alisema Mafuru.

Mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero unatarajiwa kuchukua miezi 25 kukamilika, ukitarajiwa kukamilika mnamo Julai 2023. Mradi huo wa upanuzi utanufaisha sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ujenzi, kilimo, viwanda na usafirishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles