ILIPOISHIA…
Nikiwa katika tafakari, ghafla aliingia mwanamke mmoja mrefu, mweusi mwembamba. Alikuwa msichana, si mzuri wa sura lakini umbo, ngozi nzuri ambayo naihusudu. Alikuwa mweusi ambaye hakuwahi kuuchuna uso wake kwa vipodozi. Alisimama wima mbele yangu kisha kuchanua kwa tabasamu.
SASA ENDELEA…
NILIYAONA meno yake meupe yaliyopangana na kuacha upenyo wa mwanya mzuri mdomoni kwake. Nilibaki kumkodolea macho. Nilijaribu kutafakari kwa kasi lakini sikuweza. Taratibu akiwa kasimama tayari alitorokwa na neno alilolituma kwangu.
“Mbununu, unajisikiaje?” aliniuliza dada yule.
Alikuwa muuguzi katika hospitali ile. Nilijaribu kuitika kumjibu, cha ajabu sauti yangu haikutoka. Nililazimika kulisafisha koo kwa kikohozi chepesi.
Nilihisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kimeganda kooni na kuitowesha sauti yangu. Niliufungua mdomo wangu kujibu tena. Nilikusudia kujibu na kueleza kisha kuuliza yale ambayo nilipaswa kuyauliza.
Sikuwa najua nini ambacho kilikuwa kikiendelea. Kwa pingu miguuni na mkononi nilijua kuwa tayari nilikuwa chini ya uangalizi wa wanausalama hasa jeshi la polisi.
Dada yule baada ya kuwa amelitua beseni la huduma za siku, alinisogelea akiwa na sindano mkononi. Tena sauti ilimtoka akinisemesha kwa upole.
“Mbununu, sindano ya mwisho. Naona unaendelea vizuri. Leo tutakuruhusu kutoka. Tofauti na siku tatu zilizopita, tulijua hutapona tena,” alizungumza muuguzi yule.
Nilitaka kusema kumjibu, cha ajabu nilivyoufungua mdomo wangu kutaka kuzungumza, sauti yangu haikutoka. Tayari muuguzi yule alinieleza tena: “Mbununu huwezi kutoa sauti tena. Itakuchukua muda mrefu kuweza kufanya hivyo.
“Kwa uchunguzi, dawa ulizokuwa umezimeza ziliathiri mfumo wako wa sauti, hivyo kwa bahati itachukua muda mrefu sana ili kuweza kurudi katika hali yako ya kawaida. Wakati fulani inaweza kwenda kimoja na usiwe na uwezo wa kutoa sauti tena.”
Nilistaajabu sana. Mwongeaji mimi, mpiga domo sokoni na baranarani hata vijiwe vyote vya kahawa kwa sauti yangu kali, siwezi tena kuzungumza.
Sikukoma.
Nilijaribu tena na tena, lakini mambo yalikuwa si mambo, sauti haikutoka wala haikukusudia kutoka zaidi ya hewa tu iliyochomoka badala ya maneno hata matamshi.
“Pole sana Mbununu,” alizungumza muuguzi yule baada ya kuwa amenidunga sindano sehemu ya kalio langu la kushoto.
Kwa kuwa sauti ilinihama, niliitika kwa kukitingisha kichwa changu ambacho kilikuwa bado kimevurugwa na kile kilichokuwa kikiendelea.
Muuguzi yule alitoweka, kama mwanafarasi wa mfalme. Nilimkagua chini hadi juu akiwa katika vazi lake jeupe. Alionekana kupanda hewani kuikaribia dari.
Alikuwa akielekea mlangoni. Kabla hajaufikia mlango alikumbuka jambo. Aligeuka kisha kuanza kurudi hadi sehemu niliyokuwa nimejilaza. Alifika akakishika kitanda kisha aliinama kuniambia kitu:
“Usiwaze sana, maana utaweza pia kuyapoteza maisha yako ama kupandwa na wazimu wa maisha. Usiyakumbuke ya zamani. Kumbuka ya sasa na yajayo lakini si kwa ubaya.”
Wakati akiongea, nilimsikiliza, macho yangu haraka yaliuendea mkono wake wa kushoto. Niliukazia macho, juu yake kwenye kidole cha pete palikuwepo pete mbili, moja ya uchumba na nyingine ilikuwa ya ndoa.
Kweli alikuwa mke wa mtu mwenye ndoa yake. Nafsi iliniuma. Tayari hisia za maisha ya furaha, mimi na Latifa zilijaa akilini. Nilikumbuka sana siku namvisha pete ya uchumba mbele ya wazazi wake.
Naikumbuka siku ambayo ilikuwa maalumu kwa ndoa, siku niliyomvalisha Latifa pete ya ndoa katikati ya umati mkubwa wa watu. Nyuso zetu zilivyokuwa na faraja pia bashasha.
Mtima wa moyo wangu ulichomwa mkuki. Nafsi iliniuma. Kumbukumbu la mauaji lilinijaa kisha machozi nayo yalinitoroka toka machoni kwangu.
Majuto ni mjukuu. Nilikuwa nimeua watu wasio na idadi lakini kwa haraka ni wawili kwa mkono wangu. Lakini je, Latifa kama angeishi, angeweza kuzaa wana wangapi?
Je, mwana Tumaini tumboni kwa mama yake angelizaliwa angekuwa nani hapa duniani? Je, angeweza kuwa na uzao wa aina gani duniani. Je, Ndisa alistahili hukumu ile?
Je, uzao wake ulikuwaje duniani? Basi kwa maswali hayo na mengine lukuki, nilikuwa mtu wa majonzi makubwa. Kwa kulia pia kwa nung’uniko. Sikuwa na wasaa wa kutubu kwani mambo yalikuwa yametokea.
Niliwaza sana.
Katikati ya tafakari zangu za majuto, macho yangu niliyaangaza kuutazama mlango wa chumba kilichonihifadhi. Niliwaza kutoroka.
Nia ya kuwa mtoro ilinifuma. Nilipoyahesabu makosa yangu, hakika hofu ya kupatiwa adhabu kali ilinijaa. Ningeanzaje kutoroka nikiwa na pingu kote miguuni na mkononi?
Nilijitutumua kisha kuketi upande upande. Niliunyanyua mkono wangu kuzitazama pingu zilizokuwa zimeung’angania mkono wangu kama ruba. Nilijaribu kuing’ata kwa meno yangu ili itanuke.
La hasha!
Ilizidi kukaza na kuusaga mkono wangu. Sikuwa nazijua pingu kwa hakika. Nilikuwa nikizisikia tu kwa mazungumzo ya vijiweni pia kupitia runinga mbalimbali za mapigano na uhalifu ambazo askari walikuwa wakiwatia nazo watuhumiwa wenye hila.
Muda ule zilikuwa mkononi kwangu. Sikuwa na haja ya kuuliza juu yake. Nikiwa bado nafurukuta, ghafla askari aliingia. Alikuwa na chupa ya chai mkononi, mfuko wa nailoni mweusi ambao baada ya kuivuta harufu kulikuwemo vitumbua.
Aliniletea chai.
Nilimtazama usoni, hakutabasamu wala kuonesha hisia za kutaka kuzungumza nami. Nilimtazama kwa kumkazia macho, niliukagua mwili wake haraka. Juu kisha chini.
Salale!
Alikuwa amebeba bunduki yake kama begi. Ilitanda mgongoni na kujishikiza ubavuni. Matumaini yalinihama.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.