Na John Wisse – 0655 618 385
NDUGU na rafiki yangu, salaam!
Nakusabahi kwa hekima, pasipo chembe ya kinyongo, kwa uungwana wako. Uyasomayo hapa ni ya kwangu, rafikiyo katika maandishi na sanaa. Naitwa Mbununu, kijana, umri wangu miaka 30.
Kiu ya maisha yangu! Kiu yangu isiyoweza kusahaulika juu ya dunia, iliugeuza wema wangu na kuwa simulizi yenye simanzi. Ingawaje wahenga walisema, ‘…ya kale hayanuki, yaliyopita si ndwele heri kuganga yajayo’ kwangu ni vigumu kuyasahau. Ya kale yananuka na yaliyopita kwangu bado ni ndwele, siwezi kuyasahau.
Hayawezi kuwa maisha yangu halisi kama nitaipuuza hii kumbukumbu muhimu na nasaba katika uhai wangu. Kizazi changu, hata kama kingepita miongo maelfu, bado kumbukumbu juu ya maisha yangu ingeingia ndani ya shajara na simulizi za wajukuu na vitukuu vyangu.
Hisi zangu pasipo subira za utu zilinifanya niyaishi maisha ya hamaniko, yenye kila aina ya changamoto zisizopimika.
Naukumbuka usiku ule. Usiku uliokuwa usiku, usiku wa giza nene lisilo nyota angani. Kila pahala usiku ule ulijaa na kuushibisha mji wa Bagamoyo kwa giza.
Taa zilizowaka kwa mwanga wa kufifia ndizo zilionekana kuhangaika kulizuia giza kuushika mji mzima na kuufanya mateka wake.
Allah! Kwa macho yangu makavu, yaliyojaa ujasiri wa kisasi, nilikatiza mtaani kwa kasi, yote nilijihimu kwenda kuikata kiu yangu. Kiu ya damu. Wakati nikiangaza macho yangu kila upande usiku ule, niliona dhahiri wakazi wa mji huo maridadi wa kitalii, walikuwa wamejifungia ndani ya majumba yao.
Hakuna aliyekuwa akirandaranda mtaani, nilijua usiku ule ulikuwa mwema kwangu. Niliunyanyua mkono wangu uliokuwa na saa iliyokuwa ikinikonyeza kila wakati, saa 5 usiku ilinieleza.
Haraka miguu niliichepua, kushoto kisha kulia miguu yangu iliniongoza kwa kasi. Panga langu jipya lililonolewa lilisimama kiunoni, nilikusudia kuikata kiu.
Ingawaje kwa wengi muda ule ulikuwa mwanana kwa kupumzika na kutafakari changamoto na baraka za kutwa nzima, kwangu ilikuwa kinyume chake.
Cha kushangaza, katikati ya giza hilo nilikuwa taabani nimefumwa na kiu iliyolitowesha lepe la usingizi. Sikuwa na hamu ya kujivika shuka kisha kuunyosha mwili wangu kitandani. Nilikuwa mtu wa kiu, kiu ya damu.
Jina langu Mbununu Mjuha Kilaza, kijana maarufu muuza ndizi. Baba wa familia yenye mke mmoja, mvuja jasho kwa kazi za juakali. Kwangu usiku na giza vilikuwa msaada mkubwa, niliwaza na kuwazua vile ningeweza kuitowesha kiu yangu iliyonifuma mfululizo na kuitowesha furaha yangu.
Miguu yangu kama mbwa mwitu, haikutulia ardhini. Nilitembea kwa kasi hatimaye nilifika maskani ambapo nilipaita kwangu. Haraka niliusogelea mlango wangu wa bati, kono langu liliugonga nikingoja kufunguliwa. Nilivuta funda na sigara yangu kubwa kisha kuuachia moshi kwenda zake kupitia tundu za pua na mdomo.
Mapigo ya moyo wangu yalikuwa mashindanoni, yalipokezana kwa kishindo cha ajabu. Masikio yangu kama jani la mgomba, yalisimama wima kusikiliza kama kulikuwa na mtu yeyote aliyekuwa akija kunifungulia.
Kimya!
Kwa nini ilikuwa kimya namna ile? Kwa nini hakuna mtu aliyekuwa tayari kunifungulia mlango? Yalikuwa maswali yangu yaliyojaa mashaka. Tayari mzizi wa wivu wenye chembe ya kuibiwa ulinijaa akilini.
Uvumilivu ulinitoroka ukaishi kwa kuelea hewani. Kwa haraka nilirudi nyuma hatua chache kisha kuuvaa mlango kwa konde. Paaa! Ilikuwa sauti ya mlango uliokuwa tayari umeng’oka na kuiparamia sakafu ya sebule yangu.
Ghafla sauti ya kwanza niliisikia ikihoji kwa hofu: “Nani wewe?” Mbununu kama faru niliyejeruhiwa, nilichepuka kwa haraka pasipo kusema neno. Moja kwa moja kama mshale, panga mkononi nikiangaza kila kona kama kulikuwa na mtu asiye wa kwangu.
Patupu!
Nilisimama wima mbele ya mke wangu aliyekuwa kaketi kitandani, wakati huo nilikuwa nikihema kama mtu aliyebebeshwa zigo zito kwa uzani. Macho kodo, niliyakodoa. Nilimtazama kwa jicho la kiama kisha naye kuingiwa wasiwasi.
“Baba Tumaini, kulikoni mume wangu?” yalikuwa maneno ya mke wangu.
Mke wa ndoa isiyoweza kuvunjika hadi kiama. Alinitazama kuanzia usoni hadi unyayo katikati ya mwanga hafifu wa taa iliyokuwa chumbani. Jasho lilinitiririka kisha kusafiri hadi chini ya nyayo zangu.
Jicho lake halikukoma kunikagua, alinitazama mkononi kwa makini, panga. Haraka aliingiwa taharuki kwa hali ambayo hakuwahi kuiona ikitokea.
Mng’aro wa panga ulimtisha na kumfanya aunyanyue mguu kukimbia akielekea sebuleni. Sikutaka kufanya ajizi. Kono langu la kushoto lilimdaka na kumshika titi lake refu lililokuwa limesitiriwa na kanga. Kwa haraka nilimchota ngwala iliyojaa ujazo, kisha chini alianguka.
Sauti kali alianza kuzitoa akiomba msaada. Shetani si shetani, bedui si bedui, kiu yangu ni kuua. Kwa haraka nilimwendea akiwa bado sakafuni na kulikaba koo lake.
Mkono wangu wa kuume uliivuta kanga yake nyepesi iliyomsitiri kisha kuisokomeza ndani ya domo lake lililonichosha. Alibaki mtupu, kama mwanasesere mbele ya duka la urembo. Nafsi yangu ilinituma kusema ungali mwili ulinitikisika kwa hasira.
“Buriani wasalimie, mwanaharamu msaliti,” maneno hayo yalinitoka ungali mkono wangu wa kuume ulilichota panga kwa haraka.
Macho yalimtoka akijaribu kujinusuru.
Kwa hasira zilizonishona, nililitazama tumbo lake lililokuwa limetuna kisha kuzipandisha pumzi na kuzishusha kwa haraka.
“Msaliti kifo halali yake. Jalali atanisamehe,” nilinong’ona na nafsi yangu.
Niliunyanyua mkono wenye panga hewani kisha kulitua shingoni kwake.
Je, nini kitaendelea? Usikose kuendelea na mkasa huu wa kusisimua Jumamosi ijayo.