24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

KITWANGA AITWANGA SERIKALI

MBUNGE wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM)

 

 

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

MBUNGE wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM), amesema atawahamasisha wananchi wa jimbo lake, wakazime mtambao wa maji ulioko katika chanzo cha maji cha Iherere, kilichoko jimboni kwake.

Kitwanga alitoa onyo hilo jana, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa na waziri wa wizara hiyo, Mhandisi Gerson Lwenge.

“Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu hakuna maji ya uhakika na tangu mwaka 2008 wananchi wamekuwa wakiyasubiri bila mafanikio.

“Kwa hiyo, nitakachokifanya safari hii, sitatoa shilingi kwenye bajeti, bali nitakwenda kuwahamasisha wananchi wa Misungwi wapatao 10,000, twende tukazime mtambo katika kile chanzo cha maji ili wote tukose.

“Wananchi wa Misungwi hawana maji, katika bajeti yenu leo mmesema Nyang’omango kuna maji wakati hakuna,  nawaambia, sitatoa shilingi nita-mobilize (hamasisha) wananchi tukazime ule mtambo.

“World Bank  (Benki ya Dunia), walifika pale kijijini wakasema hawa wananchi walioko kwenye kile chanzo wanatakiwa kupata maji, nyie hamwoni, hivi nyie mkoje?

“Nakipenda chama changu, nampenda Rais wangu Magufuli, lakini lazima tutendeane haki kwa sababu hii nchi ni yetu sote.

“Hamuwezi kupeleka maji sehemu nyingine kwa gharama ya shilingi bilioni 600, halafu mkashindwa kuwapa wananchi wangu hata mradi wa shilingi bilioni 10.

“Mshukuru nilipokuwa waziri nilikuwa siwezi kusema kitu, sasa nimetoka, tutapambana kwa sababu lazima tuwe na mipango mizuri ya kuwapelekea wananchi wetu maji kama inavyofanyika katika umeme kupitia REA (Wakala wa Umeme Vijijini),” alisema Kitwanga.

Katika maelezo yake, Kitwanga ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kabla hajafukuzwa na Rais Dk. John Magufuli mwaka jana, alilalamikia tabia ya baadhi ya viongozi wa wizara hiyo, kukwamisha upatikanaji wa maji kupitia kwa marafiki zake kutoka Austria.

“Rais alipokuja hapa, aliwaambia wananchi, kwamba nina marafiki zangu huko nje wanaoweza kunisaidia kupata maji.

“Ule mradi ulipokuja, nikawekewa figisu wakasema mimi nina interest (maslahi) nao. Ni kweli nina interest nao kwa sababu wananchi wangu wa Kolomije wanahitaji maji, wananchi wa Bukumbi wanahitaji maji.

“Kwa hiyo, mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena, safari hii sitatoa shilingi, nitakwenda kuwahamasisha wananchi wangu tukazime ule mtambo wa maji ili wote tukose,” alisisiza Kitwanga.

Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alimtahadharisha Kitwanga, kwamba kuwahamasisha wananchi ili wakavunje sheria ni kosa la jinai, hivyo awe makini kwa kuwa anaweza kuchukuliwa hatua kabla hajawahamasisha.

NDEGE

Agosti, mwaka jana Kitwanga aliiponda Serikali juu ya ununuzi wa ndege mpya kutoka Canada kwa ajili ya kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Kitwanga alisema ndege hizo, si tu hazina mwendo lakini pia ilikuwa ni ajabu kununuliwa kwa fedha taslimu wakati duniani kote ndege hununuliwa kwa kulipa kidogo kidogo wakati mteja akiendelea kuzitumia.

Serikali ilinunua kwa Bombardier Aerospace  kwa fedha taslimu ndege mbili za Q400 zinazotumia injini ya pangaboi zenye uwezo wa kubeba abiria 70.

Kitwanga amewatupia lawama watendaji wa Shirila la Ndege la ATCL akidai kuwa ndio walishauri vibaya na kusababisha kasoro katika manunuzi hayo.

Mei 20, mwaka jana, Rais Dk. Magufuli alitengua uteuzi wa Kitwanga ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa na kushindwa kujibu maswali ya wabunge kwa ufasaha.

ZITTO KABWE

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ( ACT-Wazalendo), aliwahamasisha wabunge washirikiane kuikwamisha bajeti hiyo ili ikaandaliwe upya baada ya kuwekwa mipango imara ya kukabiliana na uhaba wa maji nchini.

Kwa mujibu wa Zitto, bajeti iliyowasilishwa na Waziri Lwenge, haina mambo mapya na kwamba haionyeshi nia ya kutatua kero ya maji ambayo yamekuwa yakiwasumbua wananchi kwa miaka mingi.

“Rais alipokuja hapa bungeni, alieleza jinsi Serikali yake ilivyojipanga kuwatua akina mama ndoo kichwani. Pia tumekuwa tukiona jinsi Makamu wa Rais ambavyo amekuwa akizunguka nchini kuhakikisha anawatua ndoo kichwani akina mama.

“Pamoja na jitihada hizo, nimeshangaa kuona katika bajeti ya waziri, fedha za maendeleo zimepungua kutoka shilingi bilioni 915 za mwaka uliopita hadi kufikia shilingi bilioni 623.

“Kwa hiyo, waheshimiwa wabunge, njia pekee ya kuifanya Serikali iwe na mikakati ya kutatua kero ya maji, ni sisi hapa kuungana kwa kuikataa bajeti hii ili ikaandaliwe upya na kuja na majibu ya kutatua kero ya maji.

“Kama wewe mbunge una kero ya maji kijijini kwako, wilayani kwako, jimboni kwako na mkoani kwako, tuikatae bajeti hii ikaandaliwe upya iletwe nyingine,” alisema Zitto.

KAMBI YA UPINZANI

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya kambi hiyo, Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), alisema kambi yake imenusa harufu ya rushwa katika mradi wa kutoa maji katika Ziwa Viktoria na kuyapeleka mkoani Tabora katika Miji ya Nzega, Igunga, Tabora, Sikonge na Uyui.

“Mradi huu unahusisha malengo ya muda mrefu ya kuwapatia maji wakazi wapatao milioni 1.1 wa miji hiyo pamoja na wananchi walioko kandokando ya bomba kuu la mradi wa Kahama,” alisema.

WAZIRI WA MAJI

Wakati huo huo, Waziri  Lwenge, alisema Serikali imeendelea kuwahamasisha wananchi watumie teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua kwa kujenga mataki ya mfano katika taasisi za umma.

Waziri Lwenge aliyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Katika hotuba hiyo, Waziri Lwenge alisema Serikali imetoa mwongozo kwa halmashauri zote nchini, kutunga sheria ndogondogo zinazozitaka taasisi za kijamii na asasi za watu binafsi, kujenga miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua.

NAPE AIHADHARISHA CCM

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisipotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 kwa kutowapatia maji wananchi kinaweza kuondoka madarakani.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni mjini Dodoma wakati akichangoa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

“Kama chama kisipopeleka maji kwa wananchi kwa mujibu wa ilani ilivyoahidi kinaweza kuondoaka madarani,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles