Na CLARA MATIMO
MBUNGE wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kupata hati safi.
Kitwanga alisema halmashauri hiyo imekuwa ikipata hati chafu na zenye shaka kwa kipindi kirefu kutokana na ubadhirifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji
“Jambo hili ni la kupongeza kwa sababu tangu halmashauri hiyo ianzishwe mwaka 1997, imepata hati safi mbili, moja ilipata mwaka juzi na nyingine mwaka huu,” alisema Kitwanga.
Alisema watu hufanya kazi kwa kukiuka misingi ya maadili ya kazi hivyo kuiba fedha za umma na kuibua hoja nyingi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Alphonce Paul alisema halmashauri itaendela kuitunza hati hiyo kwa kufanya kazi kwa kujituma na kuwatumikia wananchi kwa ajili ya kuwapatia maendeleo.
Alisema walipelekwa wakaguzi maalumu kutokana na ubadhirifu huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Antony Masele alisema ubadhirifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji ndiyo uliisababishia halmashauri hiyo kupata hati zenye shaka na chafu.
Alisema ilifikia hatua kukusanya mapato madogo kwenye mazao ambayo yanategemewa katika mapato ya ndani.
“Mashambani tulikuwa tukiona magari mengi yakikusanya mazao lakini mapato tunaambiwa hayazidi Sh milioni 24, lakini kwa sasa tunaweza kukusanya ushuru hadi Sh milioni 120 kwa mwaka,”alisema.
Alisema mafanikio hayo ni kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanywa kwenye uongozi na idara mbalimbali na itaendela kusimamiwa kama inavyotakiwa kufikia malengo yao yaliyowekwa.