27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kituo cha mabasi Ubungo ‘kinavyotafunwa’

Katika gazeti hili toleo la jana, tuliaandika namna mapato yanayopatikana katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, (UBT) kilichopo jijini Dar es Salaam, yanavyokusanywa na kuishia mikononi mwa watu wachache huku miundombinu yake ikizidi kudorora.

Watoto walala juu ya miti
Gazeti hili lilibaini kuwapo kundi kubwa la watoto kutoka mikoa mbalimbali wamejenga makazi yao ya kudumu katika eneo hilo na kuwa sehemu ya maisha yao.

Jua linapozama watoto hao wenye umri kati ya miaka 7 hadi 15 huhamia kwenye miti michache iliyosalia baada ya iliyokuwapo awali kukatwa.

Watoto hao huitumia miti hiyo kama nyumba zao, huku wengine wachache wakilala katika jengo la kupumzika wasafiri lililopo ndani ya kituo hicho.

Watoto hao wamekuwa wakilala juu ya miti ambayo wameijengea nyumba mfano wa matundu vya ndege na wamefanya ndiyo makazi yao ya kudumu, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.

Kipara Silu (15) ambaye ametoka mkoani Mwanza alisema ameishi ndani ya kituo hicho kwa takribani miaka mitatu, huku akifanyakazi ya kuosha magari pamoja na kuokota makopo.

Mtoto mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Johnson Kalenga, mwenyeji wa Mkoa wa Arusha, alisema kazi yake kubwa ni kuosha magari, kuuza chuma chakavu pamoja na kuokota makopo.

Nasema kazi hiyo inamwingizia wastani wa Sh 30, 000 kwa siku, fedha ambazo alisema amezihifadhi kwa kuzichimbia katika shimo maalumu, ili baadaye aweze kupata mtaji wa kuanzisha biashara kubwa.

“Mimi na mjeda mwenzangu ndio tuliojenga nyumba hizo ili na sisi tupate kuishi vizuri kama watu wengine kwa sababu na sisi ni Watanzania halafu huko juu ni pazuri hali ya hewa nzuri na panatuwezesha kuona mambo mengi yanayoendelea huko chini pindi tunapokuwa juu tumepumzika”, alisema Kalenga.
Aidha aliongeza kuwa waliamua kuhamishia makazi yao juu ya miti kuepuka kulala chini kama mafungu ya samaki kama ilivyo kwa watoto wengine ambao wanalala chini.
Hata hivyo makazi hayo yameondolewa, baada ya uongozi na wasimamizi wa afya ndani ya kituo hicho kukata miti hiyo huku watoto hao wakishuhudia na kuangua vilio.
Biashara ya ukahaba
Kama ilivyo kwa watoto wa kiume, akina dada maarufu machangudoa ni wale ambao wamekuja mjini kwa lengo la kutafutiwa kazi na ndugu zao lakini wametelekezwa na kujikuta hawana pa kwenda wala kazi ya kufanya hivyo kuamua kujiingiza katika biashara ya ukahaba.
“Hapa wateja wakubwa wa hao machangudoa ni vijana waosha magari, ambao nao pia hawana makazi maalumu, huwachukua hao machangudoa na kufanya nao ngono kwa ujira mdogo.
Waziri azungumza
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii , Jinsi na Watoto, Dk. Pindi Chana alisema wizara inategemea kupata taarifa za watoto kama hao kutoka katika halmashuri na kupitia kwa maafisa watendaji ambao ndio wapo karibu nao.
Alisema serikali imekuwa ikichukua jukumu la kuwapeleka katika vituo vya watoto wanaohitaji misaada pamoja na kuwarudisha katika mikoa wanayotoka.
Kwa upande wake, Msemaji wa Halmashauri wa Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe aliliambia MTANZANIA kuwa taarifa za kituo hicho kuhusu ujenzi, mapato pamoja na matukio yanayoendelea watayatolea taarifa wakati wowote.

Wapiga debe washindikana

Uongozi umekuwa ukiendesha operesheni ya kukamata wapiga debe ambao wanatajwa kujihusisha na uhalifu na kuwapeleka mahakamani, lakini wamekuwa wakilipa faini na kurudia tena kuendelea na uhalifu wao.
Uongozi huo kwa sasa umeweka mkakati wa kuwalazimisha wamiliki wa mabasi kuwa na wafanyakazi wanne hadi sita kulingana na idadi ya magari ambao watapatiwa vitambulisho maalumu.
Ulinzi shirikishi lawamani
Vijana wanaojulikana na kutambuliwa na Jeshi la Polisi kama wasaidizi maarufu kama walinzi shirikishi wanatajwa kuwa ndiyo vinara wa wizi, uchafu, uuzaji wa bangi na mirungi ndani ya kituo hicho.
Katika wizi huo vijana hao wanadaiwa kushirikiana na baadhi ya askari ambao hugawana nao fedha wanazozikusanya kwa njia zisizo halali.
Kitega uchumi kikubwa cha walinzi hao ni kuwakamata na kuwatoza faini za papo kwa hapo wapita njia ambao hujisaidia haja ndogo eneo linalozunguka stendi hiyo ya Ubungo.
Faini hizo huanzia kati ya 30,000 hadi 50,000 kulingana na uwezo wa muhusika. Inadaiwa vijana hao huvizia wapiti njia wa usiku na kuwakamata na mtu anapokataa kutoa fedha hupelekwa kwa askari polisi ambao humtisha hivyo kuamua kutoa fedha hizo ambazo pia hazitolewi stakabadhi.
Hatua hiyo inakiuka sheria za halmashauri ya jiji ambazo kosa la uchafuzi wa mazingira faini yake haizidi Sh 10,000 lakini kikundi hicho hutoza kati ya Sh 30,000 hadi 50,000.
TABOA wanena
Mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) ambaye pia ni mmiliki wa mabasi ya Princess Shabaha, Hamza Mringo alisema kila mmliki wa mabasi anachangia Sh 1,000 kila siku kwa ajili ya kuwalipa vijana wa ulinzi shirikishi waliopo ndani ya kituo hicho.
Naye msemaji wa TABOA, Emmanuel Mrutu alisema kituo hicho kwa sasa ni kama zizi la ng’ombe kwani hakuna mazingira rafiki ya kufanyia kazi licha ya kulalamika kwa mamlaka lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
“Kile kituo kiko kama zizi la ng’ombe tu hakuna huduma yoyote na ukilinganisha kuwa tunalipia ushuru lakini hakuna mazingira rafiki kabisa ya kufanyia kazi, tumepaza sauti zetu hakuna mahali ambako hatujaenda lakini hakuna chochote tulichosaidiwa” alisema Mrutu.
Kukithiri kwa uchafu
Akizungumza na MTANZANIA, msimamizi wa usafi ndani ya kituo hicho, Mrisho Salumu alikiri uchafu kukithiri kwa asilimia 70.
Kutokana na hali hiyo, alisema wanatarajia kuendesha zoezi la kuzibua mifereji ya maji machafu yoliyotuama kutokana na uharibifu wa miundombinu iliyoharibika wakati wa zoezi la bomoa bomoa ya majengo ili kukifanyia ukarabati kituo hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles