KAMA mie sielewi unachosema na kuelewa unamaanisha nini, basi kila wakati, tutakuwa tuna matatizo. Hatutaweza kupata jukwaa zuri la sie pamoja kuweza kukutana na kujadiliana changamoto ambazo tunazikuta pamoja, zinazotukabili katika mawasiliano yetu. Hii ndio moja ya changamoto nyingiU. Hatuelewani, wakati mwingine lugha ni ngumu kweli kweli.
Sio Ughabuni tu hata hapa nyumbani watu wanaweza kuzungumza mpaka rangi inawabadilika lakini hakuna mwafaka. Na mara nyingi yote haya yanatokana na ubinafsi. Na ubinafsi unatokana na malezi. Kama ni hulka yako, malezi yataipiga msasa na kukupa msingi na mwongozo wa kimaisha kukusaidia na kukuwezesha kuipiga vita nafsi hiyo.
Ni kama dini katika jamii, kazi moja ambayo imechukua ni ustawishaji wa kazi ya jumuiya, sasa kila kitu unamuachia Mwenyeenzi akusaidie na akupe nguvu. Huu mfumo wa kukusaidia wewe binafsi na wewe uweze kusaidia jamii umetoka wapi na ni kwa lugha gani ambayo umeletwa ambayo ni ngeni na mazingira, mila na desturi zetu.
Katika malezi yetu ya kiasili au zile mila zetu na desturi za pande hizi, ubinafsi ni kitu ambacho hakipo katika malezi yetu. Utu ni kitu ambacho kilikuwa ni moja za nguzo katika jamii.
Tumekuja huku kutafuta maisha. Wengi wetu hawakuwa wanafahamu lugha, mila na desturi za huku au kufahamu maisha ya huku kabla ya kuja wameelezwa na mtu au watu. Kwa bahati mbaya au nzuri kuelezwa sio kama kuona na kuwa na uzoefu mwenyewe . Kitu gani kinakufanya wewe kuhama kutoka mazingira uliyoyazoea na kwenda nchi nyingine mbali na haufahamu mila wala desturi, ni ubinafsi.
Huku unakuta mazingira tofauti sana kuliko huko ulikotoka, mimea na mpaka hali ya hewa ni tofauti. Chakula, harufu, nguo wanazovaa au jinsi wasivyovaa, Ughaibuni Ulaya Kaskazini ni tofauti.
Kama umefika wakati wa baridi na nchi mzima ipo chini ya theluji ni kubaki kushangaa tu jinsi mazingira yalivyokuwa ni tofauti na jinsi ubaridi unavyokupiga, hakuna hata sikumoja utakuwa umejitayarishwa na mazingira ya namna hi.
Kwanza tu jinsi giza linavyo funika kama jamvi hiki kipande cha dunia na kuendela na hali hiyo mpaka mwezi wa tatu kutoka mwezi wa 10. Saa nane na nusu tayari ni giza na kupambazuka kwenye saa mbili na nusu au saa tatu asubuhi. Ni karibu masaa sita tu unapata mwanga wa jua (kama litajitokeza). Na hali hii inaenda kuanzia mwezi wa 10 mpaka mwezi wa tatu.
Baada ya miezi hiyo ni kunapambazuka kwenye saa 10 alfajiri na kwa masaa 17 na kuzama saa tatu usiku mpaka kwenye mwezi wa kumi.
Hii msifikirie kwamba inakuja mara moja tu kama unavyowasha na kuzima taa. Inakuja hatua kwa hatua mpaka kwenye kilele ambao ni mwezi Juni 21 na 22 inayojulikana kama katikati ya majira ya joto (midsummer).
Polepole baada ya hapo giza linarudi mpaka siku za mwanga zinakuwa chache na giza linatawala mpaka kufikia kwenye kilele cha giza ambapo unapata masaa machache tu ya mwanga kwenye Desemba 12. Desemba 21 au 22 na mwanga polepole kurudi mpaka kilele tena cha Juni. Hali hi ndio maisha yetu huku Ughaibuni.
Ulaya Kaskazini husherekea siku kumi na mbili msimu wa baridi. Hizi siku huita ”Julhelg” ambazo siku kama nne kati ya hizo tunaita krismasi. Mila na desturi za Ulaya Kaskazini nyumbani kwao wanaweka mti wa Krismasi, maua ya Krismasi. Haya yote yametokana na mila na desturi zao za zamani kabla ya ukristo na wakaingiza kwenye dini. Sie tukaletewa na tukaiga bila ya kujua inatoka wapi. Tunakwenda kula ”Krismasi” lakini ni mila na desturi za Ulaya ambazo zipo kabla ya imani ya kikristu.
Katikati ya majira ya joto, kwenye kilele, siku hiyo inajulikana kama Siku ya Yohana Mtakatifu (St Yohana), ni kipindi ambacho Ulaya Kaskazini wanasherekea kwa jua kuwa kwenye kilele. Hizi sherehe ni zipo hata kabla ya Ukristo kuingia. Ni kuadhimisha siku ndefu kama mapambano yasiyo ya kawaida kati ya mwanga na giza, joto na baridi.
Kati ya Juni 19 na 25 tamaduni mbalimbali Ulaya wanasherekea jua. Kanisa la Kikristo wameteua Juni 24 kama Siku ya Sikukuu Shahidi Mtakatifu John Baptist na maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Yohana Mbatizaji huanza jioni kabla Juni 23, unaojulikana kama ’Usiku wa Mtakatifu Yohana Mbatizaji’
Hizi siku ni ukumbusho kwa madhehebu mengi ya kikristo. Hizi siku zimeangukia na hizo siku ambazo jamii ya Ulaya Kaskazini wanaabudu jua na kuipiga vita giza. Wamechanganya dini na utamaduni wao.
Katika kuimarisha utamaduni wao ndani ya dini au dini ndani ya utamaduni wao wameweza kuendeleza ujuzi wao kwa vizazi vifuatavyo. Haikuwa rahisi kwani changamoto zilikuwa nyingi.
Siye ambao tumezoea jua, unakuta baada ya miaka kadhaa kuishi kwenye hali hii, bila ya kuwa na mazingira fulani kibinafsi ambao yanakusaidia kutokufikiria jinsi hali ilivyo na upweke unaofuatia, basi unyongevu fulani na huzuni hukupata na kuwa sehemu ya maisha yako.
Tengo Kilumanga
Email: tengok@gmail.com
Tel: +467051263303
Twitter: @tengo_k