WASHINGTON- Marekani
MEXICO imekubali kuchukua ‘hatua isiyo ya kawaida’ itakayosaidia kupunguza wimbi kubwa la wahamiaji kwenda Marekani ili kuepuka vitisho vilivyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump la ongezeko la ushuru wa bidhaa.
Marekani na Mexico zimekuwa katika mazungumzo kwa siku mbili yaliyomalizika jana juu ya suala hilo la kudhibiti wahamiaji haramu.
Jana kupitia akaunti yake ya Twitter, Rais Trump aliandika maandiko kadhaa, akibainisha kuwa anasitisha mpango wa kuzuia ongezeko la ushuru kwa muda usiojulikana baada ya kukubaliana na Mexico juu ya suala hilo la wahamiaji haramu.
Kama njia ya kuishinikiza Mexico kuzuia wimbi kubwa la wahamiaji wake haramu nchini Marekani, Trump alitishia kongeza ushuru wa asilimia tano kila mwezi katika bidhaa za nchi hiyo.
“Ninafurahi kukujulisha kuwa Marekani imefikia makubaliano yaliyosainiwa na Mexico. Ushuru ambao ulipangwa kutekelezwa na Marekani Jumatatu dhidi ya Mexico umesimamishwa kwa muda” lilisomeka andiko la Trump.
Makubaliano hayo ya sasa pia yalithibishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico, Marcelo Ebrard, aliyesema kwamba yamefikia mwisho baada ya siku mbili za mazungumzo yaliyoshuhudia Marekani ikihitaji kukomeshwa kwa vitendo vya wahamiaji haramu Amerika ya Kati.
Maofisa wa nchi hizo mbili walikuwa katika mazungumzo ya wakijadili mwakafa wa kuzuia ongezeko la ushuru wa bidhaa.
Katika azimio lao la pamoja lililotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, nchi hizo mbili zilisema Mexico itachukua hatua kali kudhibiti wahamiaji haramu na biashara ya binadamu.
Marekani pia imekubali kutanua programu yake ya kuwarudisha wakimbizi Mexico wakati wakisubiri malalamiko yao kupitiwa.
Nchi zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuratibu hatua fulani fulani pamoja na kushirikiana taarifa.
Pia wameazimia majadiliano kuendelea, na kwamba makubaliano ya mwisho yatatangazwa ndani ya siku 90.
Wastani wa watu milioni moja wanatajwa kupita kila mwaka katika mpaka kati ya Mexico na Marekani.