Benjamin Sawe, Dar es Salaam
LICHA ya Tanzania kuwa na utajiri wa makabila zaidi ya 120, lakini watu wake wapo katika hatari ya kuzika lugha zao za asili kwa kuwa idadi kubwa ya wazazi wanazipuuza na hivyo kuwafundisha watoto lugha ya Kiswahili pekee.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lugha za asili ni utambulisho wa makabila mbalimbali duniani na zina umuhimu mkubwa katika jamii.
Hivyo, Watanzania wanapaswa kuweka mikakati ya kuwarithisha watoto wao lugha na tamaduni zao kwa kuwa ipo tofauti kubwa kati ya ukabila na makabila. Lugha na utamaduni wa asili ni urithi usioshikika na una thamani kubwa kwa Taifa hivyo wazazi wasizipuuze kwa kisingizio cha kuepuka ukabila.
Wakati wa kupigania Uhuru wa Tanganyika, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alihimiza matumizi ya Kiswahili ili kuimarisha mfumo wa mawasiliano na kujenga Taifa lenye nguvu.
Hata hivyo alisema jambo hilo haliwazuii Watanzania kuendeleza makabila yao.
Baba wa Taifa alikuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ukabila ili kudumisha amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania, jambo lililochangia kuishi kama ndugu bila kujali tofauti za rangi, kabila wala itikadi za kidini.
Hata hivyo, Kiswahili hakipaswi kuchukuliwa kama tishio kwa lugha za asili kutokana na ukweli kwamba binadamu ana uwezo wa kujifunza na kuzungumza lugha zaidi ya tatu.
Taarifa za tafiti zinazofanywa na wataalamu mbalimbali wa masuala ya lugha na utamaduni, zinabainisha sababu zinazowafanya wazazi kutowafundisha watoto lugha za asili.
Sababu ya kwanza ni dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa lugha za asili zinajenga ukabila. Sababu ya pili ni elimu na mwingiliano wa watu katika makabila ambapo hata watoto wanaozaliwa vijijini wanalazimika kuzungumza Kiswahili wakati wote kama lugha ya mawasiliano shuleni na wanapokuwa nyumbani.
Mfumo wa maisha ya kisasa unaleta changamoto kubwa katika jitihada za kukuza lugha za asili pamoja na kudumisha mila na desturi za makabila mbalimbali nchini Tanzania. Pia mwingiliano wa makabila katika ndoa, kukua kwa miji, maisha ya kuhamahama na kukua kwa mfumo wa elimu ni miongoni mwa sababu kubwa zinazodidimiza maendeleo ya lugha za asili, mila na desturi za makabila mbalimbali.
Tofauti na miaka ya nyuma ambapo ilikuwa ni nadra kuona watu wa makabila tofauti wakioana, hivi sasa asilimia kubwa ya wanandoa ni watu wa makabila tofauti jambo linalosababisha watoto kuzungumza lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili.
Maisha ya kuhamahama yanasababisha watoto kutojifunza lugha ya asili hata kama wazazi wao wametoka kabila moja. Pia gharama za usafiri zinakwamisha maendeleo ya lugha ya asili kwa kuwa wazazi waliokuwa na desturi za kuwapeleka watoto wao vijijini wakati wa likizo hivi sasa wameacha kufanya hivyo kitendo kinachowanyima watoto fursa ya kujifunza mambo ya asili.
Kukua kwa miji na mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi kunasababishwa na watu wa makabila tofauti kuacha kutumia lugha zao za asili na kuzungumza lugha inayoeleweka na watu wote. Pia wanapohamia eneo fulani wanaacha mila na desturi za makabila yao na kufuata mfumo mpya wa maisha kulingana na eneo walilohamia.
Watanzania wanapaswa kuweka mikakati ya kufungua benki za kuhifadhi taarifa mbalimbali kuhusu mila na desturi za kila kabila nchini, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha watoto lugha za asili na kuwasimulia hadithi mbalimbali juu ya mambo ya kale hususani juu ya mila na desturi ambazo hazina madhara kwa jamii.
Kwa kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaathiri tamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali, wazee wanapaswa kutumiwa kikamilifu ili kukusanya taarifa muhimu na kuziweka katika maandishi.
Watu na viongozi wa makabila hayo wanapaswa kuweka mikakati ya kutangaza mila na desturi zao ili Watanzania kudumisha utajiri wa mila na desturi za makabila ya Tanzania.
Lugha za asili zimebeba maarifa mengi yaliyolimbikizwa na jamii ambapo kama jitihada za makusudi hazitachukuliwa sasa kuzidumisha,kuzififisha na kuzibeza zitakufa taratibu katika kipindi cha miaka 20 ijayo.
Ni wazi kwamba lugha zetu za asili zimeanza kukosa mvuto mbele ya kizazi hiki kipya ambacho sehemu kubwa ya maisha yao toka kuzaliwa na kukulia kwenye mazingira yanayotumia lugha za mataifa ya Magharibi.
Lugha hizi, lazima zifunguliwe milango katika sekta ya habari na mawasiliano, katika elimu na katika siasa. Kuthamini lugha zetu kutatupa msukumo mkubwa katika kujiletea maendeleo, kujenga demokrasia na kuhifadhi utamaduni wetu.