28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAYOPASWA KUYAFAHAMU KUHUSU SHULE ZA MSINGI ZA BWENI – 10

Wanafunzi wa bweni

Na Christian Bwaya,

TUMESHAURIANA mambo ya kuzingatia tunapolazimika kuwapeleka watoto wadogo kwenye shule za msingi za bweni. Kubwa zaidi ni mzazi kujiridhisha na namna shule inavyomwekea mtoto mazingira mazuri yanayofanana na yale ya nyumbani.

Katika makala haya, tunazishauri manajementi za shule zinazotoa huduma za bweni kwa ngazi ya shule ya msingi.  Ushauri huu unatokana na uchambuzi wa matokeo ya tafiti mbalimbali za malezi ya watoto wanaolelewa vituoni (institutionalized child care).

Huduma za msingi

Shule zihakikishe huduma zinazingatia ubora kwa kuyafanya mazingira ya shule yawe na sura ya nyumbani. Watoto wadogo wasichanganywe na watoto wa umri mkubwa katika chumba/bweni moja. Mtoto asichangie kitanda na wenzake; aishi na majirani wachache chumbani wanaolingana nae kiumri; apate uangalizi wa karibu kwa mlezi mwenye sifa na anawasiliana kwa karibu na wazazi wake.

Idadi nzuri kwa watoto wa darasa la kwanza mpaka la saba ni watoto wanne kwa chumba kimoja bwenini. Mlezi mmoja aangalie vyumba viwili mpaka vinne kwa watoto wa madarasa ya awali, na vyumba vinne mpaka sita kwa madarasa ya juu. Kufanya hivi kunawawezesha walezi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mtoto mmoja moja kama inavyokuwa nyumbani.

Sifa za walezi

Si kila mtu anaweza kuwa mlezi wa watoto wadogo. Ni muhimu basi kupata mtu mwenye moyo wa kuwapenda, kuwajali na kuwatunza watoto bila kujisikia kusumbuliwa. Mara nyingi walezi wa kike ambao ni wazazi hufanya vizuri zaidi ya walezi wa kiume. Hawa wanakuwa na uelewa mzuri wa mahitaji mahususi ya watoto kuliko walezi wasio wazazi.

Kadhalika, walezi wasibadilike badilike mara kwa mara. Watoto wanahitaji kuwa na mtu waliyemzoea na kumwamini, waweze kuwa huru naye. Unapobadili mlezi mara kwa mara, unawapa kazi watoto kumzoea upya hali inayoweza kuwafanya wakakosa amani kuona mtu waliyemwamini anaachana nao. Shule ziwaandalie walezi semina za mara kwa mara kuwasaidia kuboresha uelewa wao kuhusu mahitaji ya watoto kiumri.

Utaratibu wa mawasialiano

Mtoto aliyetengwa na familia yake anapungukiwa kitu muhimu kwenye maisha yake. Shule itengeneza utaratibu mzuri wa wazazi kuwasiliana na watoto wao mara kwa mara. Kwa watoto wa madarasa ya awali, ni vyema wazazi wapate fursa ya kuwaona watoto angalau mara moja kwa juma. Kufanya hivi kutawaruhusu watoto kuendelea kuwa karibu na wazazi wao hata katika mazingira ya shule.

Sambamba na hili, wazazi waelimishwe na kulazimika kuwatembelea watoto wao wanaoishi kama kigezo cha kuendelea kupata huduma hiyo ya bweni.

Mazingira sisimushi

Shule iweke mazingira sisimushi kwa mtoto. Sambamba na vifaa vya kujifunzia vinavyopatikana kwenye shule nyingi, ni muhimu kuhakikisha watoto wanapata muda mzuri wa kucheza na kufurahia muda wa mapumziko.

Pia shule iwe na ratiba ya kuwawezesha watoto kushiriki kazi za mikono. Badala ya kuwa na watu maalum wa kufanya kazi za nje, ni muhimu mtoto ashiriki kikamilifu. Shughuli kama kufua nguo nyepesi, kusafisha maeneo anayoishi, kutunza bustani, kusafisha vyombo na shughuli nyingine kama hizo.

Wazazi waelimishwe hasara za kuwa na matarajio makubwa kitaaluma kwa watoto wao yanayoweza kufanya shule zipunguze muda wa michezo ambayo nayo ni muhimu kwa watoto.

Inaendelea

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles