26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KIRUSI KINGINE BONGO MUVI HIKI HAPA!

Na JOSEPH SHALUWA

BADO hali ya soko la sinema za Kibongo siyo nzuri. Najua harakati mbalimbali zinafanywa ili kurejesha uhai wa sanaa na wasanii wenyewe.

Nathamini mchango mkubwa wa sanaa ya filamu ambayo imesaidia ajira kwa vijana wetu. Lakini hali ya sasa inatishia, wadau wanatafuta sababu ya myumbo ili kuirudisha kwenye hatamu.

Kwa hakika ni jambo zuri. Kwa nyakati tofauti, kama mdau wa sanaa nimekuwa nikiandika sababu za hapa na pale ninazodhani zimechangia kurudisha nyuma sanaa yetu. Naamini ni kati ya mchango mzuri utakaosaidia kuwashtua wasanii wetu.

Katika mfululizo wa maandiko yangu (nitaendelea kuandika), leo naomba nizungumzia kirusi kingine kinachotafuna sanaa yetu ili sasa wakati tutakapoamka tuwe tumepata tiba yake na kinga pia ili kisirudi tena kututafuna.

Najua si wote wanataonielewa na watakaonielewa si wote watakubaliana nami. Lakini nadhani huu ni muda sahihi wa kuzungumzia hilo, angalau kwa wachache wenye uelewa wanaweza kupokea na kuchukua hatua.

  1. SANAA KUGEUZWA UHUNI

Nianze kwa kuuuliza; hivi ni kwa nini waume wengi hawataki kusikia wake zao wakijiingiza kwenye mambo ya sanaa? Ni kwa nini binti akianza sanaa, iwe ya kuigiza, muziki au unenguaji, huonekana malaya, mhuni na asiye na staha?

Kwa nini wanaume wengi mastaa wa fani mbalimbali, wakitaka kuchumbia mahali, wazazi huweka angalizo kwa mabinti zao? Ni kwa nini wanaume wanaowaoa wasanii, huwaachisha wenzi wao shughuli za sanaa baada ya kuwaoa?

Haya maswali yanaweza kutoa mwanga wa kile ninachotaka kukizungumza hapa. Jibu ni moja, sanaa inaonekana ni uhuni. Lakini ni kweli ni uhuni? Jibu rahisi sana. Sanaa siyo uhuni ila baadhi ya waliopo kwenye sanaa wanageuza kama genge la wahuni.

Sanaa ni yenu wenyewe, mna jukumu la kuilinda na kuiheshimu kwa sababu maisha yenu yapo hapo. Wasanii na watu maarufu kwa jumla Bongo wanatia kichefuchefu kwenye suala la uhusiano wa mapenzi.

Hata kama binti alikuwa na heshima vipi, akianza sanaa tu, tarajia mabadiliko. Na huku Bongo Muvi ndiyo kichefuchefu zaidi. Dawa ni chungu lakini inaponya! Tukubaliane hapo halafu tujirekebishe.

Msichana aliyekuwa mtulivu, utamsikia kwenye kumbi za burudani kila kukicha, utamsikia akihusishwa na wapenzi tofauti kila kukicha, kisa? Eti amekuwa staa. Sanaa siyo uhuni, ni kazi.

  1. RUSHWA YA NGONO

Utakuta msanii wa kiume, anaunganisha wasanii wenzake wa kike kwenye uhusiano na anawatumia wote atakavyo. Wengine bila haya, hawataki kuwasaidia chipukizi mpaka wapewe penzi. Ni mdudu gani anawasumbua?

Zaidi nawaonea huruma wasichana. Tatizo mnashindwa kuelewa umuhimu wa mapenzi ulivyo. Mnashindwa kufahamu thamani ya kupenda na kupendwa katika maisha. Ndugu zangu, mapenzi ni ukamilifu wa maisha halisi.

Hata kama ukiwa na fedha kiasi gani, kama huna unayempenda kwa dhati na hakuna anayekupenda kwa dhati, unajiharibia furaha na burudani ya maisha yako. Hili ni jambo la kisaikolojia ambalo halionekani kwa macho.

Mtu mwenye uhusiano na wenzi wengi kwa wakati mmoja ana matatizo ya kisaikolojia. Anapoteza furaha ya ndani na uwezo wake wa kufikiri unapunguzwa na usaliti wa nafsi na wasiwasi wa kusababisha maumivu kwa mwingine. Mapenzi ni maisha.

Yupo staa mmoja (wa kike) wa filamu niliwahi kuzungumza naye huko nyuma. Nilikutana naye kiwanja usiku mnene,  alikuwa amelewa. Kwa sababu ya pombe, aliweza kuwa jasiri na kunieleza jambo zito linalomtesa.

Aliniomba jambo hilo liwe siri – ilikuwa hivyo kweli. Alinieleza huku analia, namna alivyokuwa kwenye utumwa wa mapenzi na staa mmoja mkubwa wa filamu Bongo. Alisema, pamoja na kwamba anajua kuwa ana wanawake wengine tena wengine anawajua kabisa, aliendelea kuvumilia kwa sababu alimpenda na aliogopa kuwekwa pembeni kwenye sanaa.

Wapo wengi wa sampuli hii. Wasanii mnawajua – mnajuana, listi ni ndefu sana. Mnapoteza muda kwa kushindana na kugombania mapenzi badala ya kubuni vitu vipya vitakavyozidi kuwaweka juu zaidi kwenye sanaa.

  1. SKENDO ZA MAPENZI

Wengine wanajidanganya kwamba wakiingia kwenye skendo za mapenzi na waandishi wakanasa na kuandika, watakuwa juu kisanii. Ni mawazo ya kijinga hayo.

Mastaa wa kike waliochakazwa kwenye mapenzi wanajua mateso wanayopata sasa hivi – nani ataoa mmama mtu mzima aliyekuwa akiripotiwa kubadilisha wanaume kila siku? Nani atakubali kuolewa na mwanaume ambaye kila siku anabadilisha wanawake?

Heshima yenu kwenye jamii iko wapi? Acheni uvivu wa kufikiri. Hebu jifunzeni kwa wenzenu wa Marekani, Nigeria, India na Ghana (kwa mfano). Wanaheshimu mapenzi na mara nyingi uhusiano wao huwa wa wazi.

Wana staha. Wanaingia kwenye uhusiano wa wazi, kila mtu anaujua ili isije ikatokea tatizo la kuingiliana kwenye mapenzi. Hata kama ikitokea wameachana, mambo yatakuwa wazi na baada ya muda utasikia anatoka na mwingine.

Tuendelee kutafuta suluhu ya Bongo Muvi. Tutaporejea hivi virusi tuwe tumevikabili!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles