Na Abducado Emmanuel, Dar es Salaam
MCHEZAJI bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kipre Tchetche, anayekipiga kwa mabingwa wa ligi msimu uliopita, Azam FC, amesifia ushindani wa namba kwenye nafasi yake ya ushambuliaji baada ya kusajiliwa kwa Mhaiti, Leonel Saint-Preux.
Tchetche alifanikiwa kufunga mabao 13 msimu uliopita wa ligi, pungufu ya mabao matatu aliyofunga misimu miwili iliyopita na kuibuka mfungaji bora wa ligi kwa mabao 16.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, mshambuliaji huyo mwenye mashuti makali na chenga za maudhi, alisema kusajiliwa kwa straika huyo wa Haiti kunaongeza ushindani mkubwa kwenye namba hiyo, huku akidai ni jambo zuri kwenye timu.
“Kusajiliwa kwa Mhaiti ni jambo zuri, kwani ushindani utaongezeka zaidi, tupo washambuliaji wengi hivi sasa kwenye kikosi, ni jambo zuri kwenye timu, kwani utaleta msaada mkubwa katika mafanikio ya timu yetu,” alisema Tchetche.
Kusajiliwa kwa Mhaiti huyo kunafanya Azam FC kutimiza idadi ya washambuliaji kumi, Khamis Mcha, Ismail Diara, Joseph Kimwaga, Kelvin Friday na Farid Malick (wote ni mawinga wa pembeni), John Bocco, Saint-Preux, Didier Kavumbagu, Gaudence Mwaikimba na Tchetche.