29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mwandosya autaka urais

Profesa Mark Mwandosya
Mbunge wa Rungwe Mashariki na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya

NA ELIZABETH MJATTA

MBUNGE wa Rungwe Mashariki na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, amefunguka kwa mara ya kwanza na kuelezea mwelekeo wake wa kisiasa na hasa nia yake ya kuwania urais mwaka 2015.

Mwandosya, ambaye alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, tayari ameeleza wazi kuwa hatatetea tena kiti chake cha ubunge mwaka 2015.

Akizungumzia suala la urais, Mwandosya, ambaye amewahi kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama kugombea urais mwaka 2005, akichuana na Rais Jakaya Kikwete, alisema itakuwa heshima kwake kama chama kitaweza kumfikiria na hatimaye kumteua kugombea urais mwaka 2015.

“Kuteuliwa na chama kuwa mgombea urais ni heshima kubwa na ni kilele cha utumishi ambao mwanachama anaweza kutoa kwa chama na kwa Taifa. Itakuwa ni heshima iliyoje kwangu iwapo chama kitaweza kunifikiria na hatimaye kuniteua kufika hapo,” alisema Mwandosya katika mahojiano hayo.

Hata hivyo, Mwandosya alisema tusimtake avuke daraja hata kabla ya kulifikia asije akatumbukia kwenye maji au kama mto hauna maji basi asianguke kwenye mawe.

Bila kufafanua kauli yake hiyo ina maana gani, Mwandosya alikumbusha jinsi uamuzi wake wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais mwaka 2005 ilivyomjengea heshima na kumtia moyo.

“Mtakumbuka tarehe 4 Mei mwaka 2005 nilikuwa mmoja wa wanachama watatu tuliopewa heshima kubwa ya kufika Chimwaga mbele ya Mkutano Mkuu wa CCM (Taifa). Wengine walikuwa Jakaya Kikwete na Dk. Salim Ahmed Salim. Katika uchaguzi huo Kikwete alipata tuzo ya ‘dhahabu’, Dk Salim alipata tuzo ya ‘fedha’ na mimi nikapata tuzo ya ‘shaba’.

“Niliwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu na chama kwa ujumla na kusema ‘shaba si haba’. Angalau nina mtaji wa kuanzia,” alisema Mwandosya.

Miaka miwili iliyopita, Mwandosya ambaye alikuwa akikabiliwa na maradhi, alikaririwa akisema kuwa hatakuwa tayari kuzungumzia urais na badala yake alikuwa ameelekeza akili yake katika kuhakikisha afya yake inaimarika kwanza ndipo azungumzie mustakabali wake wa siasa za 2015.

Kauli yake hiyo aliitoa mara baada ya Rais Jakaya Kikwete kumuapisha Ikulu, jijini Dar es Salaam kutokana na kuwepo nchini India kwa matibabu wakati mawaziri wapya wakiapishwa.

Akizungumzia hali yake ya kiafya kwa sasa, Mwandosya alisema anamshukuru Mungu kwa uponyaji, kwani miaka mitatu iliyopita ilikuwa ni yenye changamoto kubwa kwake.

“Ni kweli miaka mitatu iliyopita imekuwa yenye changamoto kubwa kwangu kiafya na hivyo kwa familia yangu na Watanzania  wenzangu. Kabla sijaugua ghafla mwaka  2011, nilikuwa sijawahi kulazwa hospitali.

“Nilikuwa nikienda hospitali kuwajulia hali wagonjwa. Wahenga wanasema hakika ‘hujafa hujaumbika’. Nimechukulia kuumwa kama vile ni mtihani katika maisha, kwamba binadamu inapaswa apitie ili awe kamili.

“Bila shaka unaweza kudhihirisha kwamba ile picha wakati Rais ananisaidia kushuka ngazi za Ikulu baada ya kuniapisha kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi yake na mnavyoniona sasa ni tofauti kabisa. Namshukuru Mwenyezi Mungu, muweza wa vyote kwa uponyaji,” alisema Mwandosya.

Pia alisema kuwa anawashukuru Watanzania wengi ambao walimuweka katika dua, maombi na sala.

“Sina cha kuwalipa isipokuwa kujitahidi, kwa kadri Maulana atakavyonijalia, kutoa utumishi uliotukuka,” alisema Mwandosya.

Kwa mara ya kwanza, Profesa Mwandosya alipelekwa nchini  India kwa matibabu mwaka 2011 na kurejea nchini Novemba 29, akiwa amekaa nchini humo kwa miezi mitano.

Mwandosya ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki, ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakitajwa kuwania urais mwaka 2015, baada ya kushindwa kupata nafasi hiyo alipojitosa mwaka 2005.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 na ule wa 2010 uliompa ushindi Rais Jakaya Kikwete, Profesa Mwandosya, ambaye si mzungumzaji, alipata kuhisiwa na kundi la wanamtandao akidaiwa kushirikiana na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, anayetoka naye mkoa mmoja.

Pamoja na Mwakyembe, katika kundi hilo ilidaiwa kuwa wamo pia Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta pamoja na wanasiasa wengine ambao wakati huo walionekana kujinasibu na mapambano dhidi ya ufisadi.

Hata hivyo, baada ya afya ya Mwandosya kuanza kuzorota, matumaini ya mwanasiasa huyo kuwania urais yakaanza kufifia, fursa ambayo wachambuzi na wadadisi wa mambo wanadai kuwa imechukuliwa na Sitta, ambaye tayari ameshatangaza azma yake ya kugombea nafasi hiyo mwaka 2015.

Mei 2013, Waziri Sitta akiwa kwenye  Kongamano la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St. Augustine, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa wakati ukifika, yeye na rafiki zake watachagua mmoja wao watakayeona anafaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Bila kulitaja jina la Mwandosya, Sitta aliwataja marafiki zake hao kuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Siku chache baada ya Sitta kumhusisha Dk Magufuli na kundi la urais la mwaka 2015, Waziri huyo aliibuka na kupinga kauli hiyo, akisisitiza hafikirii kuwania nafasi hiyo.

Mbali na Mwandosya, ndani ya Chama Cha Mapinduzi wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.

Wengine ni Waziri Membe, Sitta, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye tayari amekwisha tangaza msimamo wake wa kugombea urais mwaka 2015.

Katika kinyang’anyiro hicho yumo pia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Stephen Wassira, Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed Shein.

Hata hivyo katikati ya mbio hizo za urais, imeibuka hoja mpya ya ujana na uzee.

Hoja hiyo tayari imewagawa Watanzania katika makundi mawili, moja likipigia chapuo vijana na jingine wazee, kwa madai kuwa nafasi ya urais ni nyeti hivyo inahitaji mtu aliyekomaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles