Na Muhammed Khamis (UoI)-Zanzibar
CHAMA cha Wananchi (CUF) tawi la Kidatu C Jimbo la Mtoni Unguja, limemfukuza uanachama aliyekuwa kiongozi wa walinzi wa chama hicho, Thiney Juma Mohamed kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa tawi hilo, Ali Abdalla Khatib alisema kabla ya kufikia uamuzi huo, waliitisha mkutano mkuu wa wajumbe wote ambao ulimjadili kwa kina juu ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Alisema mkutano huo, ulimjadili Mohamed kutokana na taarifa yake aliyoitoa kwenye vyombo vya habari kupinga namna utaratibu wa uendeshaji wa chama unavyofanywa, huku akihusisha baadhi ya viongozi wakuu kuvunja Katiba.
“Hili ni kosa, chama chetu kina msemaji wake haiwezekani utoke na kusema kwenye vyombo vya habari wakati wasemaji wa chama wapo,’’alisema.
Alisema mkutano huo, ulimpa fursa Mohamed na alikiri kufanya hivyo, huku akiomba msamaha.
Akijibu tuhuma hizo, Mohamed alisema kitendo cha kuzungumza na vyombo vya habari si kosa, kwa sababu alitoa maoni yake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari,Unenzi na Mahusiano ya Umma, Salim Biman alisema chama hicho ni taasisi iliyo imara inayohitaji kuendeshwa kama zilivyo taasisi nyingine.
“Kilichofanywa na tawi la Kidatu C, ni sawa maana wamemwona mwanachama wao ana hatia na ndiyo maana wameamua kumfukuza,”alisema Bimani.