25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

KIONGOZI WA KAMBI YA UPINZANI KUWANIA URAIS AKIWA GEREZANI

DAKAR, SEGENAL           |           


KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani nchini Senegal na Meya wa zamani wa Jiji la Dakar, Khalifa Sall ambaye yuko gerezani kwa sasa, ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2019.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AfricaNews, Sall ametangaza nia ya kuwania urais kwa njia ya barua licha kutumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa ya kujipatia dola milioni 3.24 kwa njia za udanganyifu na kughushi nyaraka, tuhuma ambazo alikanusha na sasa anakamilisha mchakato wa kukata rufaa.

“Ni kweli, mimi ni mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Februari 24, mwaka 2019,” amesema Sall katika barua yake.

Haijafahamika kama Sall ambaye amekuwa mwanasiasa nyota anayemchachafya Rais wa sasa wa Senegal, Macky Sall, ataendelea na mpango wa kugombea iwapo rufaa yake itagonga mwamba mahakamani hali itakayomlazimu kubaki gerezani. Rais Sall na Khalifa Sall hawana undugu wowote licha ya kufanana majina ya ukoo.

Hata hivyo, inadaiwa Sall anao wafuasi watiifu, hususan katika Jiji la Dakar, huku wengi wakiamini kuwa kukamatwa kwake na kufungwa kulichochewa na mbio za urais wa mwakani.  Serikali imekanusha kuhusika na tuhuma hizo.

Kutokana na hali hiyo heshima ya Senegal katika demokrasia ipo majaribuni iwapo Khalifa Sall ataendelea kuzuiliwa gerezani hadi wakati wa uchaguzi mkuu.

Licha ya sifa kubwa ya uchaguzi wa kidemokrasia mwaka 2012, Senegal imedaiwa kuingia kwenye mtikisiko wa kisiasa baada ya kukumbwa na matatizo makubwa ya ufisadi na kukosa uvumilivu wa kisiasa.

Karim Wade ambaye ni mtoto wa zamani wa Rais Abdoulaye Wade, anatumikia kifungo cha miaka mitatu jela kutokana na makosa ya ufisadi, ikiwemo kuficha fedha ughaibuni kupitia kampuni mbalimbali zilizosajiliwa katika visiwa vya Virgin, nchini Uingereza pamoja na kashfa ya Panama papers.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles