MASHABIKI wa timu ya Simba visiwani hapa wameanza kufurahishwa na viwango vya nyota wao wapya, Paul Kiongera na Hijja Ungando, wakidai wametengeneza kombinesheni nzuri.
Ungando na Kiongera, aliyekuwa kwa mkopo KCB ya Kenya, wameanza kufanya vizuri kwenye maandalizi ya Simba kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi hii.
Akizungumza mara baada ya mazoezi ya jana, mmoja wa mashabiki hao aliyekataa kutajwa jina gazetini, alisema pacha ya wawili hao itawasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yao msimu huu, wakiungana na kinara wa mabao, Hamis Kiiza, aliyefunga nane.
“Kwa sasa yeyote aje, kwani tumetimia, tuko vizuri, imani yangu tutafika mbali, Ungando ni kijana hatari sana na ukiwatizama pamoja na Kiongera ni mapacha wapya watakaotusaidia sana ndani ya timu yetu ya Simba,” alisema.
Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, katika mazoezi ya jana alionekana kuwanoa zaidi washambuliaji, hasa Kiongera na Hijja, ambao kwa sasa ni kama pacha iliyokubalika zaidi visiwani hapa.
Kiongera tokea ameondoka Simba akipelekwa kwa mkopo KCB, ameonyesha kiwango kikubwa sana, akifunga mabao 11 msimu uliopita wa ligi hiyo, akizidiwa mabao 11 na staa aliyeongoza, Jesse Were wa Tusker.
Katika mazoezi hayo, ilishuhudiwa kiungo Awadh Juma, akishindwa kufanya mazoezi kutokana na kusumbuliwa na malaria, vilevile mshambuliaji kinda, Alex Masawe naye aliumia bega baada ya kuanguka, akiwa katika harakati za kufunga bao.
Masawe ambaye anawania namba ya kupandishwa kwenye timu kubwa ya Simba, ameumia ikiwa ni siku yake ya kwanza tu kufanya mazoezi na kikosi hicho baada ya kuwasili visiwani Zanzibar tokea juzi.