27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

SIMBA V AZAM Ni vita ya Waingereza

simba-vs-azamNA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

MTIFUANO! Ndivyo litakavyokuwa pambano kati ya vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC na timu ya Simba, mchezo utakaofanyika Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kila shabiki wa soka nchini analisubiria kwa hamu pambano hilo linalotarajiwa kuwa kali na la aina yake, kwa sasa timu zote hizo zipo bize kufanya maandalizi ya mwisho mwisho huku kila upande ukijinasibu kuibuka na ushindi.

Azam iliyokuwa imeweka kambi ya siku tano mkoani Tanga imesharejea jijini Dar es Salaam tangu juzi mchana na jana iliingia kambini kwa maandalizi ya mwisho, wapinzani wao Simba wenyewe bado wamejichimbia kambini visiwani Zanzibar.

Matajiri hao kutoka Azam Complex wataingia dimbani kwenye mchezo huo wakiwa kileleni kwa pointi 25 baada ya kuambulia ushindi mechi nane, sare moja, huku Simba iliyofungwa mechi mbili na kushinda saba ikiwa nafasi ya nne kwa pointi zao 21.

Timu zote mbili zilikuwa zikiwakosa baadhi ya wachezaji wao waliokuwa wakishiriki michuano ya Kombe la Chalenji nchini Ethiopia, Azam ikiwakosa nyota 12 na Simba saba ambao wote wamesharipoti kambini kuanzia jana.

Rekodi ya Ligi Kuu mpaka sasa inaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 14 tokea Azam FC ianze kucheza ligi hiyo msimu wa 2008/09, Simba imeshinda mechi saba, Azam mara nne na zimetoka sare tatu.

 

Vita ya Waingereza

Hakika pambano la mwaka huu baina ya timu hizo litakuwa ni la aina yake, kwani litahusisha vita ya makocha kutoka Uingereza, Stewart Hall kwa upande wa Azam na Dylan Kerr kutoka Simba.

Mpaka sasa kitakwimu, Hall anaonekana amemzidi Kerr kutokana na mwenendo mzuri wa Azam waliokuwa nao hivi sasa wakiwa hawajapoteza mchezo wowote.

Kerr aliyekuja kwa mara ya kwanza Simba msimu huu, amewahi kucheza mpira akiwa kama beki wa kushoto huku mpinzani wake Hall akirejea kwa mara ya tatu Azam msimu huu, anatambuliwa na Chama cha Soka England (FA) kama Mkufunzi wa Makocha wa Taifa hilo.

Mfumo uliompa umaarufu Hall hivi sasa na kuipa mafanikio Azam kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame Agosti mwaka huu, bila kufungwa mchezo wowote ni 3-5-2 huku pia akiujaribu mfumo mpya wa 3-4-3, ambao ni mbadala wa huo wa kwanza.

Kwa mujibu wa mechi mbalimbali za Simba msimu huu, Kerr anapendelea zaidi mfumo wa 4-2-3-1, ambapo mara chache ameweza pia kutumia mfumo mwingine wa 3-4-3. Hivyo litakuwa pambano la kimbinu zaidi.

 

Ubora

Ukizipima kwenye mizani timu hizo mpaka sasa Azam imeonekana kuwa bora sana kuliko Simba, mbali na kuwa kileleni bali ndio pekee iliyoweza kushinda kwa asilimia 100 mechi za ugenini, ikishinda zote tatu dhidi ya Stand United (2-0), Mwadui (1-0) na Ndanda (1-0).

Pia mechi ilizocheza nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, imeshinda zote nne na moja nyingine ikicheza Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Yanga inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 23 na kutoka sare ya bao 1-1.

Simba imecheza mechi nne nayo ugenini, imepigwa moja dhidi Tanzania Prisons (1-0) na kushinda tatu walipocheza na Mbeya City (1-0), Mgambo JKT (2-0) na African Sports (1-0), nyumbani imecheza tano imeshinda nne na kufungwa moja.

Azam pia inaizidi Simba kwenye ufungaji mabao ikiwa imefunga 20, ikiwa na wastani wa kufunga mabao 2.2 kila mchezo huku Wekundu hao wakitupia 15, sawa na wastani wa bao 1.6 kila mechi lakini wote wameruhusu nyavu zao kuguswa mara tano (sawa na wastani wa kufungwa bao 0.6 kila mechi).

 

Usajili/vikosi

Azam imeongeza nguvu langoni tu kwenye usajili wa dirisha dogo ikimsajili kipa Ivo Mapunda atakayekuwa akisaidiana na Aishi Manula na Mwadini Ali.

Baadhi ya wachezaji Simba iliyowasajili ni washambuliaji Paul Kiongera, Haji Ugando na Danny Lyanga huku ikiwa kwenye hatua za mwisho kumalizia taratibu za kumnasa winga wa Azam, Brian Majwega.

Mpaka sasa Azam imeng’arishwa na nyota kadhaa Kipre Tchetche mwenye mabao saba, Shomari Kapombe manne na Didier Kavumbagu, aliyecheza mechi mbili za mwisho akiwa amefunga matatu, winga Farid Maliki, pia viungo hodari Himid Mao, Salum Abubakar, Mudathir Yahya na Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’.

Simba yenyewe itakuwa ikitegemea makali ya Mganda Hamis Kiiza mwenye mabao nane mpaka sasa, Kiongera aliyerejea akitokea KCB ya Kenya, Majwega kama atafanikiwa kumalizia taratibu za usajili na baadhi ya viungo wake hodari, kama Said Ndemla, Jonas Mkude na Justice Madjavi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles