29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Kinana awarushia kombora viongozi wa Chadema

kinanaNA ELIYA MBONEA, KARATU
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ameanika ufisadi ulioko katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha, inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akihutubia wananchi katika Viwanja vya Mazingira mjini hapa jana, Kinana alisema viongozi wa halmashauri hiyo wameshindwa kuwaletea maendeleo wananchi, ingawa wamekuwa wakilaumu Serikali ya CCM kwamba haiwaletei maendeleo wananchi wake.
“Nyinyi mliochagua Chadema sijui kama mna habari kwamba halmashauri yenu imeomba kununua shamba la Shanglila ambalo mmiliki wake alikopa mkopo wa Dola za Marekani milioni nne.
“Chadema wanaosimamia halmashauri hii, wamefanya mpango wa kununua shamba hilo kwa shilingi bilioni 11, wakati deni ni shilingi bilioni sita. Hapo kuna watu wamepanga kunufaika, waulizeni mtapata habari,” alisema Kinana.
Mbali na ufisadi huo, alisema halmashauri inadaiwa kupima viwanja na kuviuza kwa Sh milioni 10.5 wakati wakijua gharama hizo ni kubwa na hakuna mwananchi wa kawaida atakayeweza kununua viwanja hivyo.
“Hata fedha za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 28 zilizotolewa na Serikali Kuu, kati yake shilingi bilioni 12 hazijulikani zimetumikaje.
“Tatizo jingine lililoko hapa ni kwamba, viongozi wa halmashauri wamewanyang’anya wananchi wa Kata ya Baray shilingi milioni 60 za ujenzi wa zahanati, wakati fedha hizo zilitolewa na Serikali Kuu,” alisema.
Huku akitahadharisha asipigiwe makofi wala kushangiliwa, Kinana alisema miradi mingi katika halmashauri hiyo imeshindwa kutekelezwa kwa kuwa madiwani wa Chadema ndiyo kikwazo.
“Wakati naelekea Kijiji cha Kilimatembo pale Rothia, nilikuta wananchi wamefunga njia ili kufikisha ujumbe kwangu, kwamba hawana maji kwa miaka mingi.
“Wananchi walisema kwamba, wakati wao hawana maji, upande wa pili anaishi Mwenyekiti wa Halmashauri, Maasai aliyejipelekea mradi wa visima vitatu kwa fedha za Serikali na amejiwekea ili wananchi wasichote maji yake.
“Huyo ndiye kiongozi wa watu maskini anayesimama jukwaani na kusema CCM ni mafisadi, hawafai na ni watu wabaya, chagueni Chadema wakati jirani zake hawana maji,” alisema Kinana.
“Nimeambiwa pia hata mlima uliopo jirani yake nao ameuuza, hiyo ndiyo halmashauri ya Chadema, mliichagua wenyewe, sasa mnasaga meno mambo yamewafika na mashitaka mnaleta kwa Katibu Mkuu wa CCM,” alisema Kinana.
Naye Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Chadema wameigeuza Karatu kuwa pango la wanyang’anyi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles