27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KINACHODIDIMIZA ZAO LA PAMBA KANDA YA ZIWA

Na ANDREW MSECHU-SIMIYU

KILIMO ni siasa, kilimo ni uchumi, hizo ndizo kaulimbiu zilizoua sekta ya kilimo nchini na hatimaye kupoteza dira huku wakulima ambao ni zaidi ya asilimia 70 wakibaki kuwa masikini.

Moja ya zao ambalo kwa sasa limepoteza dira na kuwaacha wakulima kwenye umasikini ni zao la pamba, ambalo lilikuwa limeshika uchumi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa huku viwanda vilivyotokana na vyama vya ushirika vikipata nguvu.

Kupoteza dira kwa zao la pamba kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa kulichangiwa kwa kiasi kikubwa kuyumba vyama vya ushirika ambavyo vilikuwa na nguvu kama Shirecu, Nyanza pamoja na Muungano wa Wakulima wa zao la Pamba cha Ingembenzabo.

Kutokana na zao hilo kupoteza dira Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, imetangaza azma ya kufufua zao la pamba sambamba na ufufuaji wa viwanda vya bidhaa za zao hilo nchini, ambapo vingi vilikufa kutokana na kukosekana kwa ufanisi.

 

Azma hiyo inatangazwa huku tatizo kubwa la kukosekana kwa usimamizi makini wa zao hilo likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi, huku Serikali ikitarajia mabadiliko ya haraka katika uzalishaji wa zao hilo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa katika Mkoa wa Simiyu, unabaini kwamba pamoja na matatizo ya wakulima kukimbia kilimo cha zao hilo, tatizo kubwa ni kutokuwepo kwa wasimamizi wanaoweza kuwasaidia wakulima katika maeneo yao.

Septemba 8, mwaka huu huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika kikao cha pamoja kilichofanyika mjini Dodoma, aliwaagiza wakuu wa mikoa 10 inayolima pamba nchini wasimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na kuwaongezea kipato wananchi na kuwataka maofisa kilimo kwa kila halmashauri iliyoko kwenye mikoa hiyo wahusike kikamilifu na wasiofanya hivyo waondolewe.

Majaliwa alisema ni lazima maofisa hao wawe na mpango kazi, wausimamie na watoe matokeo ya kuwa zao hilo limefanikiwa katika eneo lake, ili lichukue nafasi yake ya namba moja na kurejesha heshima ya “Dhahabu Nyeupe” kwa kuwa zao hilo ni uchumi na pia ni siasa katika mikoa ya Shinyanga, Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi na Geita.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa wasimamizi hao ambao ndio nguzo kuu katika kusaidia wakulima kuendesha kilimo cha kisasa na kufikia malengo wana ushuhuda wao.

Wasimamizi hao wanaeleza kwamba, kutokana na uhaba wa watumishi, kukosekana kwa vitendea kazi, ucheleweshwaji wa mbegu na pembejeo, ukame usiotarajiwa na ukaidi wa wakulima katika kutekeleza maagizo ya kitaalamu ndiyo kikwazo kikuu katika kutekeleza wajibu wao.

Tatizo ni nini?

Wasimamizi wa kilimo cha pamba, yaani Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), wanunuzi wa pamba, maofisa ugani na wakulima wanasema tatizo kubwa ni hali ya hewa isiyotabirika, kutokuwepo kwa wataalamu wa kilimo wa kutosha, wakulima kutofuata maelekezo na kutowajibika ipasavyo kwa bodi ya pamba.

Ofisa Ugani wa Kata ya Kasoli wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, Masawa Magoma, anasema watendaji wamekuwa wakishindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kutokana na uchache wao, pia kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha katika maeneo ambayo wanapatikana.

“Kuna matatizo mengi ambayo sisi wataalamu wa kilimo yako juu ya uwezo wetu. Kuna matatizo yanayowakabili wakulima moja kwa moja ambao ndio tunaowajibika kwao lakini tunashindwa kuwafikia kwa wakati. Lakini zaidi hasa katika maeneo ambayo tayari kuna wataalamu, bado kuna tatizo la kukosa uwezeshaji kwa upande wa usafiri na motisha, hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wetu ipasavyo.

“Hapa kwetu matatizo haya yako wazi, uongozi wa wilaya unayatambua na tumekuwa tukiwasilisha taarifa zetu kila wakati lakini hakuna ufumbuzi uliopatikana hadi sasa, kwa maelezo kuwa uwezo wa halmashauri kwa sasa ni mdogo hivyo kutulazimu kutekeleza majukumu yetu hadi pale uwezo wetu unapoishia,” anasema.

Sehemu ya pili ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 kifungu cha 22 (b) inaeleza kuwa itahakikisha inatoa elimu kwa wakulima juu ya kanuni bora za kilimo kwa kuongeza idadi ya maofisa ugani kutoka 9,558 waliopo sasa hadi kufikia 15,082 mwaka 2020 na kuanzisha vituo vya mafunzo ya kilimo na mifugo katika kila kata nchini.

Vipi kuhusu elimu kwa wakulima?

Magoma anasema katika eneo lake, anasimamia vijiji vitatu, vyenye kaya karibu 1,800, akiwa ni mtaalamu pekee akishughulikia kilimo na mifugo, hivyo kuwa vigumu kwake kuwafikia wakulima mmoja mmoja, ila kuna Kampuni ya Alliance ambao husaidia kilimo cha pamba tu.

Anasema kwa hali halisi, suala la kuunganisha wakulima na kuwapatia elimu kwa kiasi fulani linawezekana, ila suala la uhakiki wa wakulima wakati wa kuandaa mashamba na kusimamia ustawishaji wa zao hilo inakuwa vigumu kutokana na wingi wao na ukubwa wa eneo, hivyo ni vyema angekuwa na wasaidizi angalau wawili, kwa ajili ya usimamizi wa vijiji vyote.

Kwa upande wake Ofisa Kilimo wa Kata ya Kilalo, Robert Kipindula, anasema kwake pia utekelezaji wa majukumu yake unakuwa mgumu kutokana na changamoto ya ukubwa wa eneo, kwa kuwa anahudumia kata moja yenye vijiji vinne.

Anasema katika utendaji wake pia anashughulikia kilimo na mifugo, ambapo katika eneo hilo ilitakiwa wawe wataalamu zaidi ya wanne.

Mbali na hilo, anasema ukosefu wa vitendea kazi na uwezeshaji wa posho za kumwezesha kufika kwa wakulima wote kwa wakati kwani huwa ni kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Anasema changamoto hizo ndizo kubwa kwa kuwa ni kweli kuwa wakulima wengi ambao pamoja na kupewa mafunzo kuhusu namna ya kuandaa mashamba, kupanda na kusimamia zao hilo, bado hawafuati maelekezo ya wataalamu, ambayo ni kupanda kwa mistari na namna ya kupalilia na kunyunyiza dawa, bali kutumia njia zao za jadi za kutawanya mbegu ‘kusia’ hivyo wanahitaji uangalizi wa karibu zaidi.

Kauli ya uongozi wa wilaya

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bariadi, Mhandisi Wilbert Siogopi Makala, anasema bado hali ya usimamizi wa kilimo cha pamba si nzuri.

Anasema hali hiyo inatokana na kukosekana kwa maofisa ugani katika ngazi ya vijiji ambao bado ni wachache katika Wilaya ya Bariadi, hivyo huathiri ufanisi katika usimamizi na ufuatiliaji.

“Kwa upande wa kata, angalau kila kata sasa ina ofisa kilimo. Ila kwa vijiji bado ni tatizo kubwa. Kwa hiyo kwa kila mwaka tunaomba kupata maofisa hawa, lakini kwa sasa Serikali imesitisha ajira kwa muda kutokana na uhakiki wa watumishi hewa. Hivyo bado tunasubiri ufumbuzi.

“Ila tumekuwa tukikosa kutokana na uwezo wa Serikali kuajiri. Uhitaji upo mkubwa kwa kuwa lengo ni kila kijiji kiwe naye. Hawa wanahusika moja kwa moja na mifugo na kilimo. Kwa kiwango cha chini watu hawa wanasoma kiujumla. Ila kwa ngazi za juu kuna ofisa kilimo na ofisa mifugo,” anasema Makala.

Anasema maofisa hao ndio wanaohusika kuwasaidia wakulima kitaalamu, kuwasimamia wakati wa maandalizi ya mashamba, kupanda mbegu, palizi na unyunyiziaji wa dawa na kuhakikisha kwamba pembejeo zinatumiwa ipasavyo ili kupata mavuno yanayokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Anasisitiza kuwa kutokana na kukosekana kwa maofisa ugani kwa kila kijiji, suala la usimamizi na ushauri kwa wakulima linakuwa gumu kwa kuwa wachache waliopo hawawezi kuwafikia wakulima wote kwa wakati hali inayochangiwa na ukubwa wa eneo husika sambamba na kukosekana vitendea kazi ikiwamo vyombo vya usafiri.

“Hili ni tatizo kubwa. Unajua mkulima anahitaji uangalizi wa karibu. Sasa ukimtembelea leo halafu unakuja kufika eneo lake tena baada ya wiki mbili, hawezi kukusubiri. Leo utampa maelekeo ya namna ya kupanda, lakini atapanda mwenyewe.

“Hapa tuna changamoto kidogo ya wananchi kuelewa, kwa wakulima wa mazao mengine wamekuwa wakifanya vizuri, lakini bado kuna tatizo kwa wakulima wa zao la pamba,” anasema.

Ofisa Kilimo wa Mkoa

Akielezea matatizo yaliyopo, Ofisa Kilimo Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Elias Kasuka, anasema changamoto kubwa ya usimamizi inatokana na uwezo mdogo wa Serikali kuajiri maofisa ugani, kama ambavyo mkakati wa Kilimo Kwanza ulivyoainisha.

Anasema katika mkakati huo inahitaji angalau kila kijiji kiwe na ofisa ugani, ili kupeleka utaalamu na ushauri karibu zaidi na wakulima.

Anasema katika halmashauri sita za mkoa huo yaani Bariadi Mji, Bariadi, Busega, Itilima, Maswa na Meatu, mahitaji ya watumishi wa sekta ya kilimo kusaidia wakulima yanafikia wataalamu 552 lakini waliopo ni 205 tu, hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 347.

Anasema kwa sasa idadi ya maofisa ugani inayohitajika katika ngazi ya kata ni 130, lakini waliopo ni 106, hivyo kuwa na upungufu wa watumishi, yaani maofisa ugani 24, katika ngazi ya vijiji na vitongoji watumishi wa kilimo wanaohitajika ni 471 lakini waliopo ni 50 hivyo kuwa na upungufu wa maofisa ugani 421 katika ngazi ya vijiji, hivyo kuwa na upungufu wa maofisa ugani 445 katika ngazi ya kata na vijiji.

Anaeleza hata wataalamu waliopo kwa sasa hawatekelezi wajibu wao ipasavyo, kutokana na ukosefu wa vitendea kazi, ikiwamo usafiri, pia waliopo vijijini bado hawana hata posho za kuwasaidia kwa nauli, suala linalotatiza utendaji wao.

Anasema changamoto kwa sasa zinazidi kuongezeka na Serikali inatakiwa kuajiri kwa kuwa kuna watu wengi wapo mitaani, japokuwa ofisi yake inaendelea kuushauri uongozi wa halmashauri kuhusu pato lipatikanalo kutokana na ushuru wa pamba kutumika kwenye mahitaji ya kilimo, lakini bado inaonekana inakuwa vigumu kwa kuwa fedha haitoshelezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles