25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

KINA FATMA KARUME KUONGOZA KESI ZA KIKATIBA

Na ELIZABETH HOMBO -DAR ES SALAAM

ZAIDI ya wanasheria 20 wakiongozwa na Fatma Amani Karume na wanaharakati kutoka asasi mbalimbali nchini, wanatarajia kufungua mashauri kumi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Kati ya mashauri hayo 10, mawili yameshafunguliwa.

Shauri la kwanza linalohusu kutetea haki ya mpigakura, mlalamikaji ni Bob Chacha Wangwe na wakili wake atakuwa Fatma Karume.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mratibu wa umoja huo, Dk. Makongoro Mahanga, alisema shauri hilo namba 6 linapinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Uchaguzi vinavyotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwaidhinisha wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi, huku wakiwa ni maofisa wa tume hiyo.

Kuhusu shauri la pili namba 04/2018 ambalo nalo tayari limefunguliwa Mahakama Kuu, Dk. Mahanga alisema linapinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi.

Aliwataja walalamikaji katika shauri hilo ni Francis Muhingira Garatwa, Baraka Mwago na Allan Bujo Mwakatumbula wanaotetewa na Wakili Jebra Kambole.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika kuhusu namna demokrasia inavyokandamizwa, uhuru wa kujieleza na wa kufanya siasa.

“Sasa tukaomba msaada kwa wanasheria na wakawa tayari kutusikiliza, tukaanza kujumuika nao, wamekubali kutusaidia bure.

“Tukakubaliana ndani ya miezi miwili kupeleka kesi kama kumi za kikatiba Mahakama Kuu na ziendeshwe ‘live’ kwa sababu zitavutia sana wengi.

“Tunapozungumza hapa tayari tumeshafungua hizo kesi mbili, tutaendelea kufungua nyingine kadiri tunavyoandaa. Hizi mbili ambazo tumezifungua tunasubiri zipangiwe tarehe na majaji,” alisema Dk. Mahanga.

Alisema wameamua kufanya hivyo lengo likiwa ni kuzipigania haki za kisiasa na kidemokrasia kwa kuzingatia misingi mikuu ya kikatiba na kisheria.

“Katika umoja huu tupo wanasiasa, wanaharakati, mawakili na wanasheria mbalimbali kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinachoongozwa na Dk. Hellen Kijo-Bisimba, Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kinachoongozwa na Tundu Lissu na Kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu (THDC) kinachoongozwa na Onesmo ole Ngurumwa.

“Umoja wetu sisi watu 28 wa kada mbalimbali za kitaaluma ambao ni watetezi na wanaharakati wa haki za kisiasa tunaopigania haki za kisiasa nchini kupitia movement yetu ijulikanayo kama Tunadai Demokrasia Yetu, tumeona tunazo sababu na tunayo heshima ya kufanya kitu kwa ajili ya taifa letu,” alisema Dk. Mahanga.

Kwa upande wake, Wakili Fatma, alisema ameamua kuungana na wanasheria hao kwa sababu kila uchaguzi unapofanyika kumekuwa na malalamiko.

“Imefika hatua mwananchi anaona kwamba kura yake haina thamani yoyote, matakwa yake hayasikilizwi kwa sababu kuna kitu kinaitwa ‘goli la mkono’.

“Sasa suala likaja nini hasa kinachofanya goli la mkono litokee. Kuna nini hasa kwenye mfumo wa sheria zetu zinazoruhusu ‘referee’ (wasimamizi wa uchaguzi) kiasi kwamba kuna watu wanaweza kusema ‘public’ kuwa wao wana uwezo wa kushinda kwa goli la mkono.

“Sasa mimi nimepewa hiyo kazi kama mwanachama wa TLS na sijaja binafsi, nimechukua hiyo kazi na nimeichukua kuwa ni muhimu sana ili kulinda kura ya kila mwananchi.

“Tutailinda vipi kura? Kwenye mfumo wa nchi Katiba inasema; kila mmoja wetu ana haki ya kujiingiza kwenye mambo ya nchi yake ‘either direct’ au ‘indirect’, na kila mtu ana haki ya kupiga kura na ihesabiwe.

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Ibara ya 21: ‘Raia anayo haki kushiriki kufikia maamuzi ya mambo yanayomhusu yeye au taifa lake’ sasa kama watu wanaweza kupiga goli la mkono haki yako hii imetekwa.

Inaendelea……. kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya Gazeti la MTANZANIA.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles