NA AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege limekamata zaidi ya kilo 14 za dawa za kulevya katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam na Kilimanjaro (KIA) mkoani Kilimanjaro katika kipindi cha mwaka jana.
Idadi hiyo inatajwa kuwa kubwa baada ya ulinzi kuongezwa katika viwanja hivyo, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2015 ambapo kilo 3.583 za heroine zilikamatwa.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili juzi, Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Martini Otieno, alisema ripoti ya mwaka jana inaonyesha kuwa kilo 9.364 za dawa za kulevya aina ya heroine na kilo 5.73 za cocaine zilikamatwa kwa watuhumiwa 13 tofauti wakati zikiingizwa kupitia viwanja hivyo kutoka nchi mbalimbali duniani.
“Wauzaji wa dawa za kulevya wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kila kukicha, wapo wanaoficha katika soli za viatu, mfano kuna mtu alitokea Liberia alikuwa ameficha katika taulo za watoto (pampers),” alisema.
Otieno alisema baadhi ya watuhumiwa wanakamatwa na dawa hizo wakiwa wameficha tumboni, katika shanga za kimasai na mashine za maji.
Alisema kati ya watuhumiwa 13 waliokamatwa mwaka jana, kesi nne zinaendelea kusilikilizwa mahakamani, saba zipo katika uchunguzi wakati mtuhumiwa mmoja aliachiwa baada ya kulipa faini.
“Kesi zilizopo katika uchunguzi nyingi unakuta mizigo inayokamatwa imetumwa kwa njia za vifurushi, tukishaigundua wahusika wanaogopa kujitokeza, watu hao wote bado wanatafutwa na watapatikana,” alisema.
Otieno alisema katika ripoti ya mwaka 2015 ilionyesha kushuka kwa uingizaji wa dawa hizo hadi kufikia kilo 3.583 za heroine wakati mirungi iliyokamatwa ilikuwa kilo 22.
Alisema mwaka 2014 jumla ya kilo 13.913 za heroine zilikamatwa huku kilo 2.99 za cocaine zilikamatwa.
Otieno alisema kikosi hicho kimeweka ulinzi katika viwanja vyote vya ndege nchini na watu wengi wamekuwa wakikamatwa katika viwanja viwili tu kwa kuwa ndivyo vilivyopo katika miji mikubwa inayofanya biashara hizo.
“Ulinzi ni mkali katika viwanja vyote, askari wetu wanatumia weledi wa hali ya juu kupitia mafunzo wanayoyapata na umakini zaidi, naamini kwa mwaka huu unaoanza ulinzi utakuwa mkali zaidi,” alisema Otieno.
Kuhusu uhifadhi wa dawa za kulevya zinazokamatwa, alisema wana eneo maalumu la kuhifadhia zikiwa zimefungwa kwa umakini na linalindwa kwa saa 24.