30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

POLEPOLE AWATAKA WANA CCM KUJIPIMA

NA AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM


humphrey-polepoleKATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amewataka wanachama wenzake kujipima ukweli wao kwa wananchi ili waweze kuongeza imani katika jamii.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana katika Kongamano la CCM Diplomasia.

Alisema chama hicho kimepewa dhamana na wananchi kwa sababu ya imani waliyonayo na si ubora wala ufundi wa fitina.

“Tujipime ukweli wetu upoje kwa wananchi, kila tunapoongeza ukweli imani yao inaongezeka, sio fitina na kusema uongo, wananchi wametupa dhamana hii sio kwa sababu ya uongo wala fitina dhidi ya wengine.

“Mfano matokeo ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 tulipata asilimia 80 wa mwaka 2010 tulipata asilimia 61, lakini wa mwaka 2015 tumepata asilimia 58.

“Kwa matokeo haya inaonyesha kabisa hawajatuamini kwa asilimia zote, sio kwamba wametuchoka ama hawatupendi, bali wametupa kura kwa asilimia hizi ili kutukumbusha kurudi katika mstari, tukisimama vizuri watatuelewa maana tumeshaumizwa sana,” alisema.

Pia alisema chama kimeumizwa na watu ambao wengine huenda wakawa hata hawahusiki na CCM.

Alisema zamani CCM ilizoeleka kama chama cha walarushwa na kwa sasa wanachama wanapaswa kufahamu rushwa ni adui wa haki.

“Uchaguzi mdogo wa ndani ya chama unafanyika mwaka huu wa 2017, kipindi hiki mtu atakayekuja kutumia fedha zake, mali zake ama kujulikana kwake tumkatae, hakuna kusema unachukua halafu humpigii, nayo ni dhambi, tukifanya hivyo tutakuwa tumetuma salamu kwa kundi hilo la wapenda rushwa,” alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa baadhi ya wanachama wa chama hicho wana tatizo la kutokuwa wakweli pamoja na kuwa na fitina dhidi ya wengine jambo linalosababisha kufanya siasa za kuviziana.

Pia alisema ibada bora kwa wananchi ni kuwahudumia watu wenye uhitaji kama wanavyofanya chama hicho na si vinginevyo.

Alisema kuna baadhi ya wanasiasa wanabeza utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli na wengine wanamwita dikteta kwa sababu ya utendaji wake.

“Watu wanamwita Magufuli dikteta mnawasikiliza, hivi dikteta mnamjua nyinyi? Dikteta anasikiliza mtu na kutoa uamuzi, mnamjua Iddi Amin nyinyi? Yule alikuwa anasilikiliza mtu? Magufuli sio dikteta, yule ni mtumishi kiongozi, dhana hii si mpya ipo tangu mwaka 1970,” alisema.

Polepole alisema kwa sasa viongozi wa juu wapo katika mpango wa kuhakikisha chama hicho kinarudi katika mstari.

Alisema viongozi waliruhusu CCM ihukumiwe uovu kwa sababu ya watu wachache.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, alisema wanachama wanapaswa kujiandaa na safari ya mabadiliko ndani ya chama yanayoweza yakachagia baadhi ya watu kuumizwa.

“Tujitayarishe kuyasoma na kuyaelewa mageuzi ndani ya chama ili tuwe tayari kuyatekeleza, safari ya mabadiliko ni ndefu, haitokuwa rahisi na itatuathiri baadhi yetu,” alisema.

Madabida alisema kwa sasa lazima chama hicho kisukwe upya ili kuweza kuendesha siasa za kisayansi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles