NA AZIZA MASOUD -DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, amesema ripoti mpya ya watumishi wenye vyeti feki waliopo katika wizara mbalimbali na taasisi zake, inachelewa kutolewa kwa sababu Serikali haitaki kasoro iliyojitokeza katika ripoti ya kwanza ijirudie.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu katikati ya wiki hii, Dk. Ndumbaro, aliitaja kasoro isiyotakiwa kujitokeza katika ripoti hiyo mpya ni kuorodhesha watumishi walio na vyeti visivyokamilika, ambao katika ripoti ya kwanza walitajwa baada ya kuchelewa au kupuuza kuwasilisha nyaraka zao.
Alisema uhakiki huo kwa sasa upo katika hatua za kuthibitisha watumishi waliokutwa na vyeti visivyokamilika ili kuepuka kuwaweka wengine kimakosa.
“Tumeshamaliza uhakiki, hatujatangaza kwa sababu tuna wahakiki waliopatikana na ‘incomplete’ (vyeti visivyokamilika), tunataka tukimaliza tutoe majibu yasiyo na malalamiko,” alisema.
Dk. Ndumbaro alisema lengo la kufanya uhakiki wa vyeti visivyokamilika ni kuhakikisha orodha mpya itakayotolewa inawahusisha wenye vyeti feki peke yake.
“Kuna watumishi ambao tulipotangaza mpango wa uhakiki wa vyeti hawakuwasilisha nyaraka zao kwa kuwa hawakuwapo ofisini, wengine walikuwa wanaumwa na wengine walidhani yale matangazo hayana umuhimu.
“Hawa ndio tuna wahakiki mara ya pili, baada ya hapo mtu akitajwa hana cheti atakuwa hana tu kwa sababu tutakuwa tumeshajiridhisha,” alisema.
Kuhusu rufaa zilizokatwa kupitia Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) zinazowahusisha baadhi ya watumishi kati ya 9,932 waliotajwa kuwa na vyeti feki katika ripoti ya kwanza, ambao mwisho wao ilikuwa Mei 15, mwaka huu, alisema idadi hiyo itatolewa mwishoni mwa mwezi huu licha ya kwamba waliokata rufaa ni wachache.
“Idadi ya rufaa ni chache, wengi waliokata rufaa ni wale waliobadili majina, mfano mtu kaolewa kabadilisha jina, anatumia la mume wake, lakini kazini akasahau kuwasilisha vyeti vya ndoa, hizo ndizo zipo nyingi,” alisema.
Aprili 28, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alimkabidhi Rais Dk. John Magufuli majina 9,932 ya watumishi wanaodaiwa kuwa na vyeti feki.
Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais Magufuli aliagiza watumishi hao kuondoka wenyewe kazini hadi ifikapo Mei 15, mwaka huu na wasipofanya hivyo watafikishwa mahakamani.