MWIJAGE AWAPONDA WANAOBEZA DHANA YAKE YA VIWANDA

0
505
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage

 

 

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema wanaomkejeli kuhusu dhana ya vyerehani vinne kuwa kiwanda ni washereheshaji na hawajui walisemalo.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa duka la Kampuni ya Taifa ya Vifaa vya Ujenzi China (CNBM), alisema nia ya Serikali ni kujenga utamaduni wa watu kuanza kujenga viwanda vidogo vidogo.

Hivi karibuni wakati akizungumza bungeni, waziri huyo alisema mtu mwenye uwezo wa kumiliki vyerehani vinne na akajisajili, atafahamika kuwa anamiliki kiwanda.

“Bibi yangu alinifundisha jambo moja, nisilolijua nisishabikie. Kuna tatizo la watu kushabikia mambo wasiyoyajua. Tunataka kutoka kwenye utamaduni wa kuchuuza kama yule aliyeanza koroboi, lakini leo anatengeneza ‘energy server’.

“Kwahiyo ukiwa na vyerehani vinane wewe una uhusiano na Serikali ya Kijiji, diwani na mwenyekiti wa halmashauri anakujua,” alisema Mwijage.

Alitoa mfano kuwa mtu mwenye vyerehani vinne akipewa kazi ya kushona sare za shule za tarafa nzima yenye wastani wa watoto kati ya 2,000 hadi 4,000, mwaka unaofuata ataweza kununua vyerehani 16,000.

“Usikidharau cherehani, kwahiyo huyo (anamaanisha wanaomkejeli) alikuwa mshereheshaji na alikuwa hajui anamsemea nani… sasa nimemjibu mubashara,” alisema.

Kuhusu duka hilo, alisema litabadilisha mfumo wa manunuzi na kuiwezesha Tanzania kuwa msambazaji mkubwa wa saruji katika sehemu mbalimbali duniani.

“Nyaya na rangi zinazoaminika zinazalishwa Tanzania ziko hapa, sasa wanaosema bidhaa zetu hazina viwango wanazungumza viazi na mabumunda ya bibi zao,” alisema Mwijage.

Kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha tani 530 za saruji kwa mwaka wakati viwanda vya ndani vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 10.8.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here