24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kili Stars chapa hao Wahabeshi

Kilimanjaro-StarsNA MWANDISHI WETU

TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’ leo saa 10.00 jioni itakuwa ikisaka nafasi ya kuingia nusu fainali ya Kombe la Kagame pale itakapovaana na wenyeji Ethiopia kwenye mchezo wa robo fainali.

Huo utakuwa ni mchezo wa pili kwa pande hizo mbili kukutana ndani ya siku tatu baada ya juzi kuvaana katika mechi ya hatua ya makundi wakitoka Kundi A na Ethiopia kulazimisha sare ya bao 1-1.

Bao la Kili Stars lilifungwa na winga machachari Simon Msuva huku Ethiopia ikisawazisha kwenye dakika za nyongeza kupitia kwa beki Salim Mbonde aliyejifunga mwenyewe wakati akiwa katika harakati za kuokoa mpira langoni.

Kili Stars ina rekodi nzuri mpaka sasa kwenye michuano hiyo ikiwa haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa ikiambulia ushindi mara mbili dhidi ya Somalia (4-0), Rwanda (2-1) na sare walipocheza na Ethiopia.

Stars pia ina silaha nyingi nzito kuelekea mchezo huo kwani kwenye chati ya ufungaji bora inaonyesha kuwa nyota watatu wa timu hiyo, nahodha John Bocco, Elias Maguli na Simon Msuva ambao wamefunga mawili kila mmoja.

Kocha wa Kili Stars, Abdallah Kibadeni ‘King’, ameahidi kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza hadi wakaruhusu bao la kusawazsiha dakika za mwisho huku akisisitiza kuwa bado ndoto zake ni kutwaa ubingwa huo.

“Tuliwabana wapinzani wetu kwenye mchezo wa kwanza, lakini tukawazawadia bao dakika za mwisho, Ethiopia tumewaona na tunajipanga kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo,” alisema Kibadeni baada ya kumalizika kwa mchezo wa kwanza.

Kocha huyo mkongwe amenuia kuiongoza timu hiyo kutwaa taji la nne la michuano hiyo, ambalo wamelikosa kwa muda mrefu tokea walitwae mara ya mwisho mwaka 2010 kwa kuifunga Ivory Coast bao 1-0, lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na aliyekuwa nahodha Shadrack Nsajigwa.

Ukiachana na kipute hicho, mtanange mwingine wa kukata na shoka utakaopigwa mapema saa 8.00 mchana, utawahusisha mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Uganda ‘The Cranes’ waliobeba mataji 13 watakaokipiga na waalikwa Malawi ‘The Flames’.

Robo fainali nyingine mbili kali zitapigwa kesho baina ya Kenya na Rwanda, huku pambano kali zaidi likiwakutanisha watani wa jadi Sudan watakaokipiga na Sudan Kusini, likiwa ni la marudiano mchezo wa kwanza uliisha kwa suluhu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles