24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yateua Meya Manispaa ya Kinondoni

Pg 2Veronica Romwald na Ruth Mnkeni, Dar es Salaam

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Konondoni, kimempitisha Diwani mteule wa Ubungo, Boniface Jacob (Chadema), kuwa mgombea umeya wa Manispaa ya Kinondoni, huku akiwakilisha mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mgombea huyo alikuwa akiwania nafasi hiyo huku akipambana na diwani mwenzake mteule wa Kata ya Mbweni, Abdunel Elibariki (Chadema) ambaye alishindwa kutamba.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa uchaguzi huo Venus Kimei ,  alisema Jacob alishinda kwa kura 20 kati ya kura 28 zilizopigwa.

“Wagombea walikuwa wanne lakini watatu ndio ambao walikidhi vigezo, hata hivyo waliopigiwa kura ni wawili kutokana na mgombea mmoja Ndeshukurwa Tungaraza ambaye ni Diwani mteule wa Kata ya Makongo kujitoa katika hatua za mwisho,” alisema.

Akizungumza baada ya kutangazwa kushinda kinyang’anyiro hicho, Jacob alisema ana imani atashinda katika uchaguzi utakaowajumuisha wagombea wa vyama vingine kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nitasimamia kwa vitendo sera ya elimu ambayo chama chetu iliisimamia katika kampeni na jambo zuri ni kwamba hata Rais Dk. John Magufuli amesisitiza kwamba watoto wasome bure kuanzia msingi hadi sekondari.

“Hivyo ninaamini hilo linawezekana endapo tutasimamia mapato ya ndani kwa umakini nataka Manispaa Kinondoni iwe mfano katika hili ambayo tutahakikisha tunaboresha maslahi ya walimu na kuondoa kabisa michango ya aina zote,” alisema.

Alisema atasimamia kwa kuzingatia sera ya utatu akijumuisha wananchi, wanasiasa na wataalam bila kuwabagua kwani kwa pamoja watainua maendeleo ya manispaa hiyo.

Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ni mshirika wa Ukawa, kinatarajia kumsimamishwa Diwani mteule wa Kata ya Tandale, Jumanne Mbunju (CUF) ili awanie nafasi ya unaibu meya wa manispaa hiyo.

Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yenye majimbo manne, Chadema imenyakua majimbo matatu ambayo ni Ubungo, Kawe na Kibamba, huku jimbo moja la Kinondoni likienda CUF.

Kata zinazounda halmashauri hiyo ni 34 ambapo Chadema ilishinda kata 18 na kupata madiwani wa viti maalumu 7, CCM kata 11 na viti maalumu 4 na CUF ikishinda kata 5 na viti maalumu 2.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles