Na ASHA BANI
MBUNGE Mteule wa Rais, Anne Kilango Malecela amesema uteuzi wake umetokana na uwezo alionao na si vinginevyo.
Kilango ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kabla ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Dk. John Magufuli mapema mwaka jana kutokana na kushindwa kubainisha watumishi hewa, alisema anaamini uteuzi wake umetokana na uwezo pamoja uzoefu alionao katika Bunge.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Kilango alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kutambua uwezo wake wa kuchapa kazi huku akiahidi kuendelea kuwatetea wananchi wa Same Mashariki na Watanzania kwa ujumla.
“Namshukuru sana Rais kwa kutambua uwezo wangu kwa kuwa nilishawahi kuwa mbunge nina uzoefu nitaendelea kupigania maendeleo ya wananchi na jimbo langu nitapambana kwa ajili ya nchi yangu pia.
“Nina nyumba zangu na mashamba yangu huko Same hivyo nawaambia wananchi wa Same na wananchi wote kwa ujumla narudi bungeni kuwatetea,’’alisema Kilango.
Aidha alisema atafanya kazi kwa moyo wote kuwakilisha Tanzania na chama chake bila ubaguzi.
Uteuzi wa Kilango umezua maswali mengi hasa katika mitandao ya kijamii ikiwamo sababu za kufukuzwa ukuu wa mkoa kwa kutumia msamiati wa Rais Dk. Magufuli maarufu wa ‘kutumbua majipu’ na kumteua tena kuwa mbunge.
Kilango aliteuliwa juzi usiku na Rais Dk. Magufuli. Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, mbunge huyo ataapishwa kwa mujibu wa taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.