NA OSCAR ASSENGA, TANGA
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi,a Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile amesema Serikali itaweka utaratibu wa bima ya afya kwa Watanzania wote.
Alisema jambo hilo litakuwa la sheria ili kila mtu akate bima
Dk. Ndungulile, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipozundua zanahati ya St.Marrys iliyopo Kijiji cha Mivumon wilayani Pangani, inayomilikiwa na Watawa wa Cappucion.
Alisema watafanya hivyo kwa lengo zuri kutokana na Serikali kufanya uwekezaji mkubwa na hatua hiyo inaweza kuwaondoa wananchi baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo wanapougua wakiwa hawana fedha za kupata matibabu
“Sasa hivi tutakuja utaratibu wa bima ya afya kwa watanzania wote, yatakuwa ni matakwa ya sheria, utake usitake kwa Watanzania wote, lazima wawe na bima, tunafanya uwekezaji mkubwa.
“Lakini kwa sababu anadaiwa fedha pia nimekuwa hakimu wa kusuluhisha migogoro kati ya hospitali na wananchi hivyo ili kuweza kuondokana na hili tutoke hapo waende kwenye bima ya afya kwa kila Mtanzania,”alisema.
Alisema ingawa uwekezaji huo umefanywa gharama za matibabu zinazidi kukua na jamii za wananchi wengi bado ni maskini, wakaona waboresha mifumo ya bima za afya nchini kwa kuja na CHF iliyoboreshwa
“Kwa sababu tunaweza kujenga kituo cha afya, wananchi wakashindwa kupata matibabu kwa sababu ya gharamu serikali imeliona hilo na ndiyo maana tumeona tuboreshe mifumo ya bima za afya kwa kuja CHF iliyoboreshwa,“ alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah alisema kuwapo zahanati hiyo kumekuwa chachu kubwa kwa wananchi kwa vile kutasaidia kuboresha huduma za afya kwenye tarafa yao ya Madanga.
Alisema pia kutasaidia kuwaepusha kina mama kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya ikizingatiwa walikuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwamo kujifungulia njiani.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi alisema kanisa linapotoa huduma kwa jamii linaongozwa na mwanzilishi wake Yesu Kristo, kwa sababu ukisoma kwenye injili utaona jinsi alivyowaponya watu.
Alisema pia viongozi wa dini wanafurahi kushirikiana na viongozi wa serikali katika kuwahudumia watu mbalimbali kwa awamu ya tano na kila mmoja anasisimuka na hali kubwa ya kutaka kushirikiana nayo.