27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Kila la heri Yanga ya Watanzania

Kikosi cha Yanga
Kikosi cha Yanga

*Mashabiki kuingia bure, CAF yataka wasizidi 40,000

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa timu ya Yanga, leo itashuka dimbani kuvaana na TP Mazembe katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo  huo wa Yanga ambayo ipo kundi moja na Medeama ya Ghana, Mo Bejaia ya Algeria, utakuwa wa pili wa Kundi A baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria kwa kufungwa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa nchini Algeria.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm ambaye amemaliza programu ya maandalizi nchini Uturuki alisema watahakikisha wanacheza kufa au kupona kuhakikisha wanashinda nyumbani.

“Mazembe ni timu nzuri, lakini hatutaingia uwanjani kwa kuogopa, tutacheza kama tunavyocheza na wapinzani wengine tukiwa na nia ya kupata ushindi,” alisema.

Meneja wa timu ya Mazembe, Fedrick Kitenge, alikaririwa akisema kuwa Yanga bado ni timu ndogo kupambana na timu yake, hivyo wanajiona kama wamekuja kutafuta vipaji kama walivyofanya miaka iliyopita kwa Mbwana Samatta.

“Yanga ni timu ndogo kupambana na TP Mazembe, tumekuja hapa kutafuta vipaji kama tulivyofanya kwa Samatta miaka iliyopita,” alisema Kitenge.

Yanga itacheza mchezo huo ikiwa na matumaini makubwa ya kuifunga TP Mazembe mbele ya mashabiki wake lukuki ambao wanatarajia kuingia katika uwanja huo bure, baada ya kufutwa kwa viingilio.

Kufuatia hali hiyo ya kufutwa viingilio, Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), limetoa maelekezo kwamba watu watakaoingia uwanjani wasizidi 40,000.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema CAF kupitia Mratibu wa Michezo wa shirikisho hilo, Larbi Chraibi, limetoa mapendekezo hayo kwa kile walichodai kuwa ni sababu za kiusalama.

“Yanga  kuwaruhusu mashabiki wake kuingia uwanjani bure  ni maamuzi mazuri tu kwani watawapa fursa hata wale ambao kwa namna moja ama nyingine wangeshindwa kulipia viingilio, lakini tumepokea taarifa kutoka CAF wakipendekeza mashabiki watakaoingia uwanjani wasizidi 40,000,” alisema.

Lucas alisema Yanga wanapaswa kusikiliza na kuheshimu maamuzi ya CAF, kwani wenyewe walishalihakikishia shirikisho hilo kuwa wanatarajia kuwa na tiketi 40,000 za watu watakaoingia uwanjani, hivyo kuwataka kutozidisha idadi hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro, alisema kwamba mchezo utakuwa bure gharama zote zitalipwa na Yanga kwa CAF na TFF, hivyo shabiki yeyote hatakiwi kulipa kiingilio getini.

“Tunawaomba wenzetu mashabiki wa timu pinzani kutoka pande zote kusahau yaliyopita na kuungana na sisi wakati inapocheza leo dhidi ya TP Mazembe,” alisema.

Hata hivyo, Muro alisema kwamba timu hiyo huenda ikamkosa  beki  wake mpya, Hassani Ramadhani (Kessy),  aliyesajiliwa kutoka Simba kutokana na mvutano uliopo  na timu yake ya zamani.

“Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linasimamia kila kitu juu ya Kessy ili aweze kucheza kwenye mchezo huo, hivyo tunaweza kumtumia endapo tutapa mwongozo kutoka kwao,” alisema Muro.

Kikosi cha Yanga ambacho kipo kamili bila majeruhi, kitakutana na Mazembe ambayo kiuhalisia imeshuka kiwango, si kali kama timu ile iliyoshinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika miezi saba iliyopita.

Mazembe wenyewe wataingia uwanjani huku ikijivunia mchezaji wake  bora zaidi wa nafasi ya kiungo, Rainford Kalaba (29), ambaye anaweza  kuwa tishio katika mchezo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles