RAIS Jakaya Kikwete jana alitangaza rasmi kuwa kipindi chake cha urais kitakoma Oktoba, mwaka huu, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu na kuapishwa kwa rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Amesema anajiandaa kumkabidhi mrithi wake orodha ya miradi yote ya maendeleo na mikakati yake ambayo atakuwa hajaikamilisha katika kipindi chake cha miaka 10 ya kuwa madarakani.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana, wakati akitoa hotuba mbele ya maelfu ya wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, iliyofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, mkoani Mwanza.
Kauli hii ya Rais Kikwete amejibu madai ya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambayo wamekuwa wakiyatoa kwa nyakati tofauti kuwa kuna mpango unaosukwa na viongozi waandamizi serikalini kwa kushirikiana na Bunge wa kumwongezea muda wa miaka miwili ya kuendelea na wadhifa wa urais.
Katika sherehe hizo, ambazo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, CCM, majaji na mabalozi wa mataifa mbalimbali, Rais Kikwete alisema hofu iliyoonyeshwa na viongozi wa Ukawa kuwa upo mpango wa kumwongezea muda wa kuwa madarakani hadi 2017 haina msingi, kwa sababu Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, upo pale pale.
“Jana niliwaona wazee fulani (hakuwataja majina), hivi sijui wamepagawa na nini. Wanasema ooh Rais ana mpango wa kujiongezea muda madarakani. Mimi nasema uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani utafanyika Oktoba, mwaka huu,” alisema Rais Kikwete.
Katika hotuba yake hiyo ambayo aliitumia kuzungumzia mambo mbalimbali ya kitaifa pamoja na madai na maombi ya wafanyakazi, Rais Kikwete alizungumzia moja ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na walimu lililosomeka ‘Shemeji unatuachaje,’ kwa kueleza kuwa maadhimisho hayo ya Mei Mosi ya mwaka huu ni ya mwisho akiwa madarakani, hivyo mambo ambayo hajayatekeleza yataendelea kufanyiwa kazi na mrithi wake.
“Nilianzia urais Mwanza na nimemalizia urais wangu leo hapa Mwanza. Niliahidi kutengeneza ajira milioni moja katika uongozi wangu, leo hii miaka 10 naondoka madarakani nimeshatengeneza zaidi ya ajira milioni 2.65.
“Ajira hizi zipo za sekta ya umma na sekta binafsi. Lakini bado kuna tatizo kubwa la uhaba wa ajira, hasa kwa vijana wetu. Nitamnong’oneza rais ajaye azingatie kwa kuyapa kipaumbele mambo yote muhimu ya upatikanaji wa maendeleo.
“Nimefanya mambo mengi ya maendeleo katika nchi yangu kama walivyofanya wazee wangu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Kwa hiyo nitakapoishia ndipo atakapoanzia rais ajaye. Nimeanzisha Tume ya Walimu na Bodi ya Taaluma ya Walimu, ili kuwasaidia na kuwaendeleza vizuri. Kwa kusema haya nafikiri nitawaacha pazuri,” alisema Rais Kikwete
Agizo kwa makatibu wakuu
Rais Kikwete aliwaagiza makatibu wakuu wa wizara nchini kuhakikisha wanaanzisha haraka mabaraza ya wafanyakazi ili serikali iendelee kuwajibika kwa wananchi.
“Hainiingii akilini ninaposikia kuna uhaba wa fedha. Sijasikia hata siku moja viongozi wamekosa posho za vikao vyao, sasa iweje mabaraza ya wafanyakazi yasianzishwe? Kazi hii nawaagiza makatibu wakuu wote kuisimamia,” alisema Rais Kikwete.
Aanzisha Kurugenzi ya Wauguzi
Rais Kikwete jana alitangaza rasmi kuanzishwa kwa Kurugenzi ya Wauguzi nchini, ambayo taratibu zake za kujiendesha zinakamilishwa sasa na mamlaka zinazohusika.
Alisema kuanzishwa kwa kurugenzi hiyo kunatokana na kuthamini michango ya wataalamu wa idara zote, ikiwemo sekta ya afya na Serikali itaendelea kuangalia namna ya uboreshwaji maslahi ya watumishi wa Idara ya Afya ili kuwawezesha kuwa na moyo zaidi wa kujituma katika sehemu zao za kazi.
Wafanyakazi njia panda
Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, Rais Kikwete jana aliwaambia wafanyakazi kuwa siyo rahisi kutekeleza maombi ya kupandisha kima cha chini ya mishahara kutoka Sh 265,000 hadi Sh 315,000 kama ilivyopendekezo la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Alisema si rahisi kiwango hicho cha mshahara kulipwa wakati wa kipindi chake cha uongozi, isipokuwa kupandishwa kwa kiwango kidogo katika bajeti ijayo.
Rais Kikwete alisema yeye si wa kwanza kushindwa kutekeleza ahadi zake zote kwa asilimia mia moja, kwa sababu hata watangulizi wake katika wadhifa huo hayupo aliyewahi kutekeleza ahadi zake zote kwa asilimia mia moja.
“Ombi la Tucta kutaka kima cha chini kufikia Sh 315,000 halitawezekana kutimizwa mwaka huu, labda rais ajaye wa Awamu ya Tano ataweza, lakini katika bajeti ijayo wataongeza kiasi kidogo.
“Wakati naingia madarakani kima cha chini cha mfanyakazi wa Serikali kilikuwa Sh 65,000, lakini kimekuwa kikiongezwa kila mwaka na sasa kimefikia Sh 265,000, ikiwa ni ongezeko mara nne.
“Sekta binafsi kima cha chini kilikuwa Sh 48,000, lakini kutokana na jitahada za Serikali kuyabana mashirika na taasisi binafsi hivi sasa wafanyakazi wanapokea kati ya Sh 100,000 hadi 400,000 kulingana na sekta husika na aina ya kazi,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akijibu risala ya Tucta, iliyosomwa na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Nicholas Mgaya.
Kuhusu ombi la kupunguzwa kwa kodi anayokatwa mfanyakazi kutoka asilimia 12 hadi tisa, alisema serikali itakwenda kuangalia ombi hilo, lakini haiwezi kupunguza hadi kufikia asilimia tisa.
Ukosefu wa ajira
Akizungumzia tatizo la ukosefu wa ajira kwa kwa vijana, alisema ni mtihani mgumu kwa serikali na haiwezi kulimaliza bila msaada wa sekta binafsi.
Alisema moja ya ahadi zake wakati wa kampeni zilizomwingiza madarakani ni kuongeza ajira milioni moja, lakini hadi anamaliza miaka 10, amefanikiwa kuongeza ajira 2,653,544 na kuvuka lengo, ingawa bado ajira ni tatizo kubwa nchini.
“Tuondoe fikra kwamba Serikali itamaliza tatizo la ajira, kilichopa hapa ni kushirikiana na sekta binafsi na kuziwesha ili fursa za ajira ziweze kupatikana, ila kila wizara iwe na mikakati ya kuangalia suala hili.
“Kulikuwa na tatizo la ajira kwa wageni kuingia nchini na kufanya kazi za wazawa, hili nashukuru limefikishwa bungeni na kutungiwa sheria, imebaki kazi ya kutunga kanuni, naombeni kazi hii ifanyike usiku na mchana ya kutunga kanuni mapema ili kuondoa suala hilo.
“Naomba Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), shughulikieni jambo hilo la baadhi ya taasisi na mashirika kuwakataza watumishi wake kujiunga na Tucta, pia wafanyakazi toeni taarifa za manyanyaso mnayopata ili Serikali iyafanyie kazi, ingawa najua mnahofia kupoteza kibarua.
“Serikali imejitahidi kupunguza madeni ya walimu na kufanikiwa kulipa Sh bilioni 53 ya walimu zaidi ya 70,000, mpaka sasa nimeelezwa zimetengwa Sh bilioni 9 za madai ya walimu yaliyothibitishwa ambazo zitalipwa Agosti, mwaka huu, madai mengine yamekutwa na kasoro yamerudishwa katika halmashauri husika,” alisema Rais Kikwete.
TUCTA
Awali, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya, alisema licha ya malalamiko yao kuwasilishwa serikalini, yamekuwa yakifanyiwa kazi kwa kasi ndogo, kitendo ambacho kinawafanya kuendelea kufanya kazi katika mazingira magumu.
Mbali ya ongezeko la mishahara, Mgaya aliikosoa serikali kwa kushindwa kuzingatia mapendekezo yao ambayo yangefanikisha ukuaji wa uchumi wa nchi, tofauti na ilivyo sasa.
Mgaya pia aligusia mwenendo wa hali ya amani nchini kwa kueleza kuwa kuna viashiria vya kutoweka pole pole kwa amani iliyopo ambapo alisema chanzo ni watu kuachiwa kutukuza udini, ukabila, umaeneo, upendeleo na wachache kuachiwa kujilimbikizia mali na kuendeleza vitendo vya ufisadi.
Mgaya alisema kitendo hicho kinawafanya wananchi walio wengi kukabiliwa na hali ngumu ya maisha na kuwa na hasira.
Hali ilivyokuwa uwanjani
Ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba kulikuwa na vionjo mbalimbali, vikiwamo vya mabango yaliyokuwa na ujumbe kwa Rais Kikwete, hususan bango la walimu ambalo lilikuwa likimuuliza swali kwamba ‘Shemeji unatuachaje.’
Bango hilo lilikuwa kivutio katika uwanja huo kutokana na watu kushangilia, huku kila kiongozi, akiwamo Rais Kikwete, akicheka, aliwajibu kwa kusema anawaacha kwa kuwaundia baraza la kushughulia matatizo ya walimu na tume ya taaluma ya walimu.
Mabango mengi yalikuwa na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo ‘Wafanyakazi jiandikishe, kura yako ina thamani kwa maendeleo ya nchi yetu’ na mengine yakimpongeza Rais kwa kumteua Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, ambaye ameshughulikia kero ya machinga na masuala ya Jiji la Mwanza.