26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Kikwete afunguka mazito

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amewataka viongozi nchini kuacha tabia ya kujikweza mbele za watu, na badala yake kuishi kama binadamu wa kawaida, kwani kwa kufanya hivyo hakuwapunguzii vyeo walivyonavyo.

Pia amewataka wajenge hoja kutatua mambo badala ya kutumia nguvu.

Kikwete pia amewataka Watanzania kutobaguana kwa dini wala kabila na kwamba Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na ukubwa aliokuwa nao, alikuwa mtu wa kawaida mbele ya watu wengine.

Amesema kwa namna alivyokuwa anaishi na watu, mtu akikaa naye hapati hofu ya kwamba amekaa na rais.

Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam wakati wa kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

 “Ni jambo la muhimu viongozi kutambua kuwa kujishusha hakukufanyi usiwe kiongozi kwa sababu una wakati wa kutimiza majukumu yako, lakini unapokuwa na binadamu wenzako, wako kama wewe.

“Orodha ni ndefu ya mambo ya Mwalimu, kwa sisi ambao tumebahatika kuwa karibu naye, ametuachia urithi wa mambo mengi muhimu katika nyanja zote za maisha ya Watanzania sasa ni wajibu wetu kuutambua urithi huo na kuutunza.

“Baadhi ya mambo hayo yameshakuwa tunu za taifa na ndizo zinazolea taifa hili.

“Watanzania wenzangu, wanachama wenzangu wa CCM na vyama vingine vya siasa, wa rangi zote, makabila yote na madhehebu yote ya dini, tushikamane katika kusimamia tunu hii.

“Amani na umoja hauna kabila wala chama, na mtu yeyote anayepuuza mambo haya haitakii mema nchi yetu wala yeye mwenyewe,” alisema.

 Kikwete alisema Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa kwa misimamo yake ya kuheshimu na kuthamini hoja, bila kujali zinatokea upande upi.

Alisema jambo kubwa analolikumbuka kwa Nyerere ni msimamo wake wa kuhusu uhuru wa mawazo, huku akisisitiza kuwa hoja yoyote hushindwa na hoja iliyo bora zaidi na siyo kwa kutumia mabavu.

Kikwete alisema Nyerere aliamini sana katika majadiliano na uhuru wa mawazo kutoka kwa watu wa makundi yote.

“Siku zote alikuwa akisisitiza kuwa mawazo hayapigwi rungu, ila mawazo hushindwa kwa mawazo yaliyo bora zaidi. Siku zote alikuwa akipingana na wale waliokuwa wakitaka wanaotoa mawazo hasa yanayoonekana kuwa dhidi ya Serikali wabanwe au wawekwe kizuizini,” alisema.

Alitoa mfano wa mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wa mwaka 1978 ambao ulisababisha kufungwa kwa chuo na wanafunzi walilazimika kurudi makwao.

Alisema katika mgomo huo, vilisambazwa vipeperushi vilivyokuwa na mantiki za kisiasa na baadhi ya viongozi walichukulia suala hilo kama uhaini na kupendekeza waliohusika wawekwe kizuizini, lakini Nyerere alipinga suala hilo.

“Mwalimu Nyerere alikuwa hatishwi na hoja. Kila hoja iliyokuwa ikitolewa alikuwa anataka lazima ijibiwe kwa namna bora zaidi,” alisema.

Kikwete alisema katika sura nyingine, Nyerere alikuwa kiongozi asiyejikweza, aliyeheshimu na kumjali kila mtu.

Alisema katika kumfahamu kwake, alimuona kuwa mtu aliyeheshimu na kujali utu kuliko madaraka na mamlaka aliyokuwa nayo.

“Ninamkumbuka Mwalimu kama mtu aliyetambua dhamana ya uongozi, kuwa uongozi haukumfanya awe tofauti na watu wengine wasio viongozi. Alijishusha, hakuwa na makuu. Ulikuwa ukikaa naye hupati hofu kuwa uko na rais, mtu ambaye anaweza kusema huyu mweke ndani na ukapotea.

“Alikuwa mtu wa kawaida asiyejikweza mbele ya watu wengine, kuanzia katika mavazi hadi katika uhusiano na watu, hakuwahi kuonyesha umwamba kwa sababu ya dhamana ya uongozi,” alisema.

DARASA KWA NYERERE

Kikwete alisema kutoka kwa Mwalimu, alijifunza kuwa kwa kiongozi kujishusha hakumpotezei mamlaka wala sifa yake, wala hakumfanyi asiwe kiongozi.

Alisema kuwa alijifunza pia kwamba unapokuwa na majukumu yako ya kiongozi, hiyo haimfanyi mtu awe tofauti na wengine anaowaongoza au kumpa umwamba.

Katika suala jingine, Kikwete alisema Nyerere alipenda sana vijana na aliyetambua umuhimu wa kuwajenga, ili kuwarithisha nafasi za uongozi.

“Mwalimu alitupenda sana vijana na alitupa fursa na nafasi za kujifunza uongozi, tena sio wa chini, uongozi wa juu,” alisema.

Alisisitiza kuwa wakati wote Nyerere alikuwa akisisitiza kuwa kuwapa vijana fursa na nafasi za uongozi si hisani kwao, bali ni hisani kwa chama na kwa Serikali.

NYERERE NA VYAMA VINGI

Kikwete alisema miongoni mwa mambo ambayo Nyerere alikuwa na mchango mkubwa ni katika kujenga hoja ya kuingia katika vyama vingi mwaka 1992 ambapo ni asilimia 20 ya Watanzania walipendekeza mfumo huo.

Alisema wakati wajumbe wengi wakitaka wengi waliokuwa na imani na Serikali ya chama kimoja waliofikia asilimia 80 ndio wasililizwe, kwa Nyerere mtazamo wake ulikuwa tofauti.

“Nyerere alieleza kuwa kwa kuwa bado walio wengi wana imani na Serikali na chama ndio ulikuwa wakati sahihi kuingia kwenye mfumo huo kuliko kusubiri hadi idadi ya wasio na imani iongezeke.

“Kwa wakati huo Nyerere alijenga hoja ambayo hatimaye ilikubalika, kuwapa walio wachache.

“Msingi wa hoja yake ulikuwa kwamba iwapo tutaingia katika kipindi hicho ambacho wengi bado wana imani, tutaweza kuendelea kudumu, lakini tukisubiri kuingia wakati idadi ya wasio na imani imeongezeka, ndo tunakwenda kuondoka hivyo, kwa hiyo hoja ikapita,” alisema.

Kikwete alisema suala jingine kwa Nyerere ni moyo wake wa upendo na kujitolea, uliomsukuma kuacha kazi ya ualimu yenye mshahara na kuingia katika siasa huku akiwa hana uhakika wa mafanikio wala mshahara.

“Ilikuwa kazi ngumu kwa Mwalimu kuacha ualimu, kazi yenye mshahara na kuingia kwenye shughuli isiyo na malipo kwa matumaini tu kwamba iko siku tutapata uhuru, ambayo hata hujui ni lini.

“Ukumbuke kwamba wakati huo alikuwa baba wa familia, alikuwa tayari mama Maria yuko pale na baadhi ya watoto wake tayari walishazaliwa,” alisema Kikwete.

Alisema karama alizojaliwa Nyerere zilikuwa za kipekee na ndizo zilizomwezesha kuendesha harakati za kudai uhuru kwa maneno na tukapata uhuru kwa maneno bila kumwaga damu.

Awali, akitoa taarifa ya chuo, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila alisema chimbuko la chuo hicho ni Chuo cha Uongozi cha Kivukoni kilichoanzishwa Julai 1961.

Alisema nchi ilipoingia katika mfumo wa vyema vingi mwaka 1992, chuo hiki kilianza kumilikiwa na Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles