TRA yahimiza ushirikiano taasisi zinazofanya kazi mipakani

0
452

Mwandishi wetu, Mbeya

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Edwin Mhede, amezitaka taasisi zinazofanya kazi mipakani kushirikiana kwa kuwa lengo la Serikali ni kurahisisha biashara mpakani na kuongeza mapato ya kodi yanayotokana na biashara hizo.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa TRA wa vituo vya forodha vya Kasumulu na Ipyana vilivyopo Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, mpaka wa Tanzania na Malawi.

Dk. Mhede alisema taasisi za Serikali zinazofanya kazi mipakani zinategemeana, na hivyo ni vema watumishi wa taasisi hizo kuwa na mawasiliano ya karibu ili kuweza kurahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa shughuli za kila siku mpakani za kurahisisha biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Ni vema mkawa na vikao hata vya kunywa chai pamoja ili kuimarisha uhusiano na mawasiliano na wenzenu wa taasisi nyingine zilizopo hapa mpakani ili kurahisisha utendaji kazi na kuongeza tija katika kazi zenu,” alisema.

Dk. Mhede aliwataka watumishi wa taasisi hizo kutambua kuwa wamepewa dhamana ya kusimamia shughuli za Serikali katika mpaka wa Kasumulu na mipaka mingine, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kufanya kazi kwa bidi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kurahisisha ufanyaji wa biashara mipakani.

“Ningependa kila mtumishi atambue umuhimu wake kwa taifa hili na dhamana aliyopewa kwa masilahi ya Watanzania walio wengi,” alisema.

Taasisi zinazofanya kazi katika mpaka wa Kasumulu ni Idara ya Uhamiaji, Shirika la Viwango (TBS), Wakala wa Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Tume ya Nguvu za Atomic (TaEC), Jeshi la Polisi, Idara Afya, Kilimo, Uvivu, Mifugo, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Wakala wa Vipimo (WMA)

Kituo cha Forodha na Ushuru wa Bidhaa Kasumulo kinahudumia mizigo na abiria kutoka nchi za Malawi,  Afrika Kusini, Zambia, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo (DRC) na nchi nyingine kusini mwa Afrika.

Takwimu zinaonyesha katika kipindi cha Julai 2016 hadi Septemba mwaka huu, tani 243,145 zenye thamani ya Sh bilioni 567 zimesafirishwa kwenda nchi mbalimbali za SADC kupitia mpaka wa Kasumulu na tani 145,937 zenye thamani ya Sh bilioni 233 ziliingia nchini na jumla ya Sh bilioni 47.4 zilikusanywa kama kodi katika mpaka huo pekee.

Aidha Dk. Mhede aliwapongeza watumishi wa TRA kwa kufanya kazi kwa bidii na kufanikiwa kukusanya Sh trilioni 1.767 katika kipindi cha mwezi Septemba, mwaka huu pekee, makusanyo ambayo hayajawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.

“Nia ya Serikali ni kujitegemea kwa kukusanya mapato ya ndani, hivyo sasa ni lazima tufanye kazi kwa bidii tukusanye zaidi ya hiyo Sh trilioni 1.7 ili tuvuke lengo la makusanyo na kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema Dk. Mhede.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here