27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Zahera: Tupeni yeyote tumchape

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

WAKATI droo ya mechi za  mtoano ya kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi  Kombe la Shirikisho Afrika imepangwa kuchezeshwa leo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ametamba kuwa, kikosi chake kipo tayari kumkabili mpinzani yeyote watakayepewa na kumshinda.

Yanga iliangukia hatua hiyo, baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika na Zesco United ya Zambia, kwa kuchapwa jumla ya mabao 3-2, katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini ya raundi ya kwanza.

Ilianza kulazimishwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam , kabla ya kukubali kichapo cha bao 2-1, katika mchezo wa marudiano uliochezwa Ndola, Zambia.

Baada ya kutupwa Shirikisho, vijana hao wa Jangwani wataanzia hatua ya mtoano, wakianzia nyumbani, ambapo mchezo wa kwanza utapigwa Oktoba 27, mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kabla ya marudiano kuchezwa Novemba 3, mwaka huu.

Shirikisho la Soka Barani Afrika (Caf), limefanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa michuano hiyo, ambapo sasa timu zinazotolewa raundi ya kwanza ya Ligi Mabingwa Afrika hutua hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho na huko hucheza michezo miwili  ya nyumbani na ugenini.

Timu hizo 16 zilizofurushwa Ligi ya Mabingwa, huwekwa kapu moja na nyingine 16 zilizofuzu raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, ili  kuwania kufuzu hatua ya makundi.

Droo hiyo itakuwa ya wazi kwa maana,  timu zote 32 zitawekwa chungu kimoja ili kusaka 16 zitakazounda makundi ya manne.

Orodha kamili ya timu zilidondokea Shirikisho zikitoka Ligi ya Mabingwa ni Yanga, Horoya (Guinea), Enyimba (Nigeria), Gor Mahia (Kenya) ,KCCA (Uganda), Asante Kotoko (Ghana), UD Songo (Msumbiji), Elect –Sport (Chad), Cano Sport Guinea ya Ikweta na Al Nasir ya Libya.

Nyingine ni Fosa Juniors (Madagascar), FC Nouadhibou (Mauritania),  Côte d’Or FC (Shelisheli), ASC Kara (Togo) na Green Eagles ya Zambia.

Zilizofika hatua hiyo baada ya mapambano tangu raundi ya awali ni RS Berkane (Morocco), Al Masry (Misri,) Hassania Agadir (Morocco), Zanaco (Zambia), Enugu Rangers(Nigeria) na Djoliba Athletic Club  ya Mali.

Nyingine ni Paradou AC (Algeria), ESAE (Benin), DC Motema Pembe ( Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo), FC San Pedro (Ivory Coast), Pyramids (Misri), Bandari (Kenya), Bidvest Wits (Afrika Kusini), TS Galaxy (Afrika Kusini), Proline (Uganda) na Triangle United ya Zimbabwe.

Zahera aliliambia MTANZANIA kuwa hana shaka kumvaa mpinzani yeyote kwani anaamini ana kikosi bora kinachoweza kumpa matokeo mazuri na kutinga hatua ya makundi.

“Tunajua kesho (leo) tutamjua mpinzani wetu, tunasubiri kwa hamu na baada ya hapo tutaanza mara moja maandalizi kuhakikisha tunafanya vizuri.

“Hatuiogopi timu yeyote, hadi tunafika hatua hii ujue tuko tayari kwa mapambano, hivyo kila atakayekatiza mbele yetu atakuwa halali yetu, tuna timu ambayo inaweza kukabiliana kimataifa, hicho ndicho kinachotupa sababu ya kujiamini zaidi.

“Tutaanzia nyumbani tena, jambo muhimu ni kushinda ili tujiwekee mazingira mazuri ugenini, tumejifunza kutokana na makosa tuliyofanya Ligi ya Mabingwa, hivyo tutakuja kivingine kwenye Kombe la Shirikisho,” alisema Zahera.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles