Mwandishi wetu
Kikundi cha Nguvikazi katika Kijiji cha Buanga, Kata ya Rusoli kimetoa msaada wa chakula katika shule ya msingi Bwenda ambapo kikundi hicho kimetoa kilo 220 za mahindi kwaajili ya chakula cha wanafunzi.
Akielezea historia ya kikundi hicho Mwenyekiti wa kikundi hicho Tore Masamaki amesema kuwa kikundi hicho kilianza na wanachama 18 na baada ya kupata mafanikio ya kuridhisha wanachama waliongezeka na kufikia 30.
Amesema kikundi hicho kinashirikiana na Shirika la PCI ambalo moja ya malengo yake makuu ni kutoa chakula katika shule kwaajili ya wanafunzi.
“Kupitia kikundi hiki mavuno yanayopatikana hupelekwa shuleni na mengine ni kwa manufaa yao wenyewe na familia zao, sasa tunatafuta vifaa vya umwagiliaji ili tuanze Kilimo,” amesema Masamaki.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya Bwenda Christopher Cosmas , amekiri kupokea msaada huo ambapo amesema kuwa chakula kinachotolewa shuleni hapo kimepunguza utoro na kuongeza hamasa ya wanafunzi kupenda masomo.