PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amelazimika kuahirisha kikao cha uchaguzi wa naibu meya wa jiji hilo baada ya kujitokeza malumbano yaliyosababisha kikao kuvunjika.
Kikao hicho ambacho kilianza Saa 4:00 asubuhi kilitawaliwa na malumbano hadi ilipofika saa 8:30 mchana ambako Meya Mwita alilazimika kukiahirisha uchaguzi uweze kufanyika siku nyingine.
Kuibuka kwa malumbano hayo kulitokana na kauli ya Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana kueleza kwamba wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni 23, ambao walipaswa kumchagua naibu meya pamoja na wajumbe wa kamati mbalimbali za jiji.
Alisema ofisi yake ilipokea jina moja la mgombea wa CCM, Mariam Lulida na kuwa aliyekua akishikilia nafasi hiyo kutokana Chama cha CUF, Mussa Kafana, alikihama chama chake na kuhamia CCM jambo lilomuondolea uhalali wa kuwania nafasi hiyo.
Baada ya maelezo hayo, madiwani wa Ukawa walipinga uamuzi huo wakidai CUF ilibadili jina na kumteua mgombea wa nafasi hiyo, Farouk Mohamed.
Walisema barua ya utambulisho wa mgombea huyo iliwasilishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji, Septemba mwaka huu lakini cha ajabu mkurugenzi huyo aligoma kuipokea.
“Ushaidi wa barua yetu ya kumtambulisha mgombea wa naibu meya ninayo, lakini cha ajabu mkurugenzi amekataa kupokea na kushindwa kutoa sababu,” alisema Mtolea.
Baada ya hoja hiyo aliinuka tena Mkurugenzi Liana na kueleza kwamba barua hiyo ilichelewa kufika katika ofisi yake na kumfanya mgombea huyo kukosa vigezo vya kuwania nafasi hiyo.
Kwa sababu hiyo alisema mgombea anayetambulika ni wa CCM na kuwaomba wajumbe wa kikao hicho kupiga kura waweze kumchagua.
Kauli hiyo ilipingwa tena na Mtolea na kumtaka mkurugenzi kuwaonyesha wajumbe kifungu cha sheria kinachoonyesha mgombea wa CUF amekosa sifa ya kuwania nafasi hiyo.
Hali hiyo ilisababisha Meya Mwita kuingilia kati malumbano hayo na kumwambia Mkurugenzi Liana kuwa alikuwa anavuruga uchaguzi huo.
Alimtaka Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), kutoa ufafanuzi wa sheria kama mgombea wa CUF anakubalika katika sheria au au la.
Mdee alisema mwongozo uliotolewa na Tamisemi ambao unasimamia uchaguzi wa madiwani unaeleza kwamba mwisho wa kupokea barua ya mgombea ilikuwa juzi (jana) hivyo basi kitendo cha mkurugenzi wa jiji kukataa kupokea barua ya CUF ya kumtambulisha mgombea ni kinyume na sheria.
Hata hivyo Mkurugenzi Liana aliupinga mwongozo huyo na kusisitiza kuwa mgombea ni mmoja.
Hali hiyo ilisababisha malumbano kati ya Meya na Mkurugenzi .
Meya alimtaka mkurugenzi asiharibu kikao kwa kupitisha mambo anayoyataka yeye bila kufuata sheria za uchaguzi.
Mkurugenzi naye alimtaka meya kutomwingilia na kudai yeye ndiye msimamizi wa uchaguzi huo.
Kutokana na hali hiyo, madiwani walitoa hoja ya kutaka kura zipigwe kwa siri lakini zihesabiwe wazi ili kila mmoja aone.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Meya akisema kuwa wajumbe waliokuwapo ni 23, hivyo ipigwe kura ya siri na zihesabiwe wazi kuepusha wizi wa kura.
Hoja hiyo ilipingwa na Mkurugenzi Liana aliyedai kuwa kura ya siri atahesabu yeye na hakuna mtu atakayeruhusiwa kuziona wala kuweka mawakala wa kuhesabu kura.
Hali hiyo iliibua tena malumbano ya kupinga hoja iliyotolewa na Mkurugenzi Liana huku wakimshutumu alikuwa anataka kuiba kura.
Malumbano hayo yalimfanya Mbunge wa Kigamboni ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, kumwomba Meya Mwita kuahirisha kikao uchaguzi huo ufanyike siku nyingine kwa sababu tayari umevurugika.
Hoja hiyo iliungwa mkono na madiwani na kumfanya Menya Mwita kuahirisha mkutano huo wa uchaguzi wa naibu meya hadi siku nyingine.